Nafasi Ya Matangazo

February 08, 2025













WATUMISHI wa Wizara ya Madini na Taasisi zake wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na uzalendo ili kulinda uchumi wa nchi usiweze kuathirika na mabadiliko ya sera za mataifa ya nje.

Akizungumza leo Februari 8, 2025 katika Bonaza lililoandaliwa na Tume ya Madini na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), lililofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa amesema Tanzania ina kila aina ya rasilimali ni vyema kuzitunza, kuzithamini na kutanguliza uzalendo mbele ili uchumi wa nchi uendelee kuwa imara.

“Nchi za Falme za Kiarabu wametajirika kwa rasilimali moja tu ya uchimbaji mafuta, sisi tuna kila kitu, madini ambayo tumepewa dhamana kubwa ya kusimamia tufanye kazi kubwa kama timu kwa ushirikiano, amesema Naibu Waziri Kiruswa.

Amesema, ili kufikia lengo la asilimia 10 ambalo Sekta ya Madini inapaswa kuchangia katika Pato la Taifa ni lazima  kufunga mkanda.

“Tunapaswa kufunga mkanda ili kufikia lengo la asilimia 10, siku zilizobaki si nyingi ingawa tumepiga hatua kiasi kikubwa,”amesema, Mhe. Dkt. Kiruswa.


Awali akizungumza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewataka watumishi kuendelea kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa bidii na kujituma, ili Sekta ya Madini iwe na mchango mkubwa katika taifa na kuleta unafuu kwa wananchi.


Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo amewasihi watumishi katika Sekta ya Madini kutunza afya kwa kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Aidha, Lekashingo amekabidhi tuzo maalum kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo kutokana na utendaji wake uliotukuka, busara zake na ukarimu wake na kuaminiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye Januari 15, 2025 alimthibitisha rasmi kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini.

Wakati huohuo Naibu Waziri Kiruswa ametoa  tuzo na zawadi mbali mbali kwa viongozi wastaafu ikiwa ni pamoja na kuwaaga rasmi aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume  ya Madini, Profesa Idris Kikula na Profesa Abdulkarim Mruma aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Madini.

Katika hatua nyingine washindi wa michezo mbalimbali wamekabidhiwa vikombe na medani

Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini ni  Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) na  Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI)
Posted by MROKI On Saturday, February 08, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo