Mwanyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe.Timotheo Mzava akizungumza wakati wa majumuisho ambapo alisema kamati yake imejionea na kuridhishwa kwa hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa maktaba hiyo pamoja na maendeleo ya chuo hicho.
.
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhidhwa na ujenzi wa mradi wa maktaba ya Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) ambao umefikia asilimia 99 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari 2025.
Akizungumza wakati wa majumuisho mara baada ya ziara ya kukagua ujenzi wa maktaba hiyo Februari 8, 2025 mjini Tabora, Mwanyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe.Timotheo Mzava amesema kamati yake imejionea na kuridhishwa kwa hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa maktaba hiyo pamoja na maendeleo ya chuo hicho.
“Kwa ujumla Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii baada kupitia, kukagua, kupata taarifa na kujionea kwa macho, imeridhishwa na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na uongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja Chuo cha Ardhi Tabora katika kukamilisha jengo hili la maktaba” amesema Mhe. Mzava.
Aidha, ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha Shilingi milioni 500 Septemba 2024 ambayo ilipitishwa na Bunge katika bajeti ya mwaka 2024/2025 ili kukamilisha ujenzi wa maktaba hiyo na kuleta tija kwa kuwa utasaidia vijana wanaosoma katika chuo hicho.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda ameishukuru kamati hiyo ambayo ndiyo yenye dhana ya kuisimamia, kushauri, kutoa maelekezo mbalimbali na kufuatilia kazi zinazotekelezwa na wizara hiyo.
“Wajumbe wa kamati hii wameridhika na kazi ambayo imefanyika na wanasisitiza jengo hili lianze kufanyakazi mara moja. Sisi wizara tumeiahidi kamati kuanzia tarehe 01 Machi, 2025 wanafunzi wataanza kutumia vyumba hivi kwa ajili ya huduma ya maktaba” amesema Naibu Waziri Pinda.
Akiwakaribisha wajumbe wa Kamati hiyo mkoani Tabora, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Chacha amesema miradi mingi ya maendeleo inatekelezwa na Serikali katika mkoa huo na kuihakikishia kamati hiyo kuwa Ofisi yake itahakikisha miradi yote inakamilika ukiwamo mradi huo wa ujenzi wa maktaba ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Akitoa taarifa kwa kamati hiyo, Mkuu wa Chuo hicho Bw. Jeremiah Minja amesema maktaba hiyo ilianza kujengwa mwaka 2014 na itakamilika mwezi Februari 2025 ambapo hadi sasa umegharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 2.2 za Kitanzania
.
0 comments:
Post a Comment