Nafasi Ya Matangazo

October 06, 2024


Na Mwandishi Wetu, Karatu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Degratius Ndejembi ameelekeza mkazi wa Karatu mkoani Arusha mwenye viwanja Block 'J' mzee Desderi Damiano kuendeleza eneo hilo kwa shughuli za maendeleo kufuatia halmashauri ya wilaya ya Karatu kushindwa kumlipa fidia.

Waziri Ndejembi ametoa maelekezo hayo wakati alipotembelea na kujionea eneo la viwanja hivyo  mara baada ya kuwasikiliza wananchi wa Karatu Mjini wakati wa Kliniki ya Ardhi iliyofanyika mjini humo Oktoba 5, 2024 na kuwataka watumishi wa Ardhi katika halmashauri hiyo kuwahudumia wanachi kwa wakati tofauti na Bw. Desderi ambaye suala lake ni la zaidi ya miaka 14 tangu mwaka 2010.

"Huyu ndiyo mmiliki wa asili, hajawahi kulipwa fidia kwa nini mnamzuia kuendeleza eneo ambalo ni mali yake?  Eneo hili ni la kwako mpaka watakapothibitisha tofauti, endelea na kazi zako kama ulivyokuwa umepanga" amesema Waziri Ndejembi.

Mmliki wa eneo hilo alizuiliwa kuliendeleza viwanja vyake  licha ya Halmashauri hiyo ya Karatu kutomlipa fidia katika eneo lake  lililopangwa kwa ajili ya matumizi ya eneo la wazi.

Aidha, Waziri Ndejembi ameelekeza Afisa Ardhi Joseph Madangi Jumatatu Oktoba 2024 aripoti kwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu aeleze alipataje Hati ya Miliki katika eneo linalodaiwa ni la wazi na kuendelea na ujenzi na Afisa Mipango Miji Dismas Ngole hapaswi kuwa Karatu eneo lenye thamani kubwa ya ardhi.

Awali Waziri Ndejembi ametoa hati miliki za ardhi kwa wanachi waliofika katika Kliniki ya Ardhi iliyofanyika viwanja vya Mazingira Bora vilivyopo kwenye mji wa Karatu mkoani Arusha.

Akimkaribisha Waziri Ndejembi, Mkuu wa Wilaya ya Karatu Bw. Dadi Kolimba amesema, watayatekeleza maelekezo aliyoyatoa Waziri na kuyafanyia kazi.

Amesisistiza kuwa, wataendelea kusimamia sekta ya ardhi aliyoieleza kuwa, ni mhimili wa sekta ya kilimo ambayo wananchi wanajishughulisha na kilimo cha mahindi, vitunguu, Ngano na mbaazi sambamba na  shughuli za utalii ambazo wilaya yake ina hoteli 74 za kitalii na uchimbaji madini eneo la Endabash.

Naye Mbunge wa Viti Maalum Jimbo la Karatu Cecilia Pareso amesema mahitaji ya ardhi ni muhimu na ni lazima yawe na mipango bora ambapo wananchi wanapswa kupata haki yao ya kumiliki ardhi ili kufaidi matunda ya nchi yao.









Posted by MROKI On Sunday, October 06, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo