Na. Mwandishi Wetu
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)
imewaasa watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura kutekeleza
majukumu yao kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya
uandikishaji.
Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa (Mstaafu)
Mbarouk Salim Mbarouk wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa
Daftari ngazi ya mkoa na halmashauri za
mkoa wa Dodoma leo tarehe 14 Septemba, 2024.
“Vifaa hivi (vya uboreshaji wa Daftari)
vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo
mengine ya uandikishaji nchini. Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi
kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu.,” amesema
Jaji. Mbarouk wakati akisisitiza umuhimu wa kutunza vifaa hivyo.
Amewaasa watendaji hao kuzingatia maelekezo
yote yatakayotolewa na Tume ili waweze kuyafanyia kazi wakati zoezi
litakapokuwa limeanza.
Wakati huohuo, akifungua mafunzo kama hayo
mkoani Singida, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Dkt. Zakia
Mohamed Abubakar amesema matokeo bora ya zoezi la uboreshaji wa Daftari
yatatokana na Matokeo bora ya zoezi hili yanategemea uwepo wa ushirikiano
mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji, serikali, vyama vya siasa na wadau
wengine wa uchaguzi.
“Ninawasihi muwe na ushirikiano mzuri na wa
karibu na Tume wakati wote mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu na ikiwa
mnahitaji ufafanuzi au maelekezo yeyote, msisite kuwasiliana na Tume,” amesema
mjumbe huyo wa Tume.
Mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni maandalizi
ya Mzunguko wa tano wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao
utajumuisha mkoa wa Dodoma katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Halmashauri za
Wilaya ya Bahi, Chamwino na Kongwa, mkoa wa Manyara katika Halmashauri ya Mji
wa Mbulu na Wilaya ya Kiteto na Simanjoro na mkoa wa Singida.
Uboreshaji wa daftari kwenye maeneo hayo
utaanza tarehe 25 Septemba, 2024 hadi tarehe 01 Oktoba, 2024 na vituo vitakuwa
vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Posted by MROKI
On Sunday, September 15, 2024
No comments
0 comments:
Post a Comment