Jeshi la Polisi lingependa kuwajulisha
kuwa, kama tulivyo wapa taarifa iliyokuwa na ahadi ndani yake majira ya saa 6
usiku tarehe 9.12.2025 kuamkia leo tarehe 10.12.2025 kuwa, kwa ushirikiano na
Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama tutaendelea kuimarisha hali ya usalama
nchini na kwamba tutaendelea kulinda maisha ya wananchi na mali zao, nitumie
fursa hii kuwajulisha kuwa, kazi hiyo tumeifanya vizuri na kwa ufanisi mkubwa
na hali ya usalama wa nchi yetu imeamka ikiwa shwari.
Aidha, kama tulivyo waeleza
tarehe 3 na 5 Disemba 2025 kwenye taarifa ya Jeshi la Polisi kuwa, wanaohamasisha
maandamano wanayoyaita ya amani na yasiyo na kikomo kuwa, miongoni mwa mbinu za
kihalifu 13 walizo kuwa wanahamasishana na kupanga kutumia kupitia klabu za
mitandaoni na njia zingine ni kuhakikisha wanasimamisha shughuli zote za
kiuchumi na kijamii nchini zisiendelee.
Tumewafuatilia kwa karibu na
kwa muda mrefu toka jana tarehe 9.12.2025 kwenye klabu hizo za mitandaoni na
njia zingine walizokuwa wana tumia kuwasiliana wakipanga na kuhamasishana kwa
vile jana tarehe 9.12.2025 walishindwa kufanya maandamano yao hayo yaliyo
kinyume na Katiba ya nchi ya Mwaka 1977 na Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi
wajitokeze mitaani leo tarehe 10.12.2025 kufanya maandamano hayo haramu.
Jeshi la Polisi linaendelea
kuwakumbusha, kuwasisitiza na kuwaonya wasifanye hivyo kwani wanacho kiita
maandamano ya amani yasiyo na kikomo yalipigwa marufuku toka tarehe 5.12.2025
kwa sababu yamekosa sifa kulingana na matakwa ya Sheria mama Katiba ya nchi ya
1977 na Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi Sura 322.
Jeshi la Polisi kwa
ushirikiano na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama tuna wahakikishia wananchi
tutaendelea kulinda usalama wa nchi yetu, sambamba na maisha na mali zenu ili
muweze kuendelea na shughuli zenu kama kawaida.
Aidha, kama kuna ambaye
atajitokeza na kukaidi kutii sheria za nchi kwa lengo la kuhatarisha usalama wa
nchi ili kusimamisha shughuli za kiuchumi na kijamii zisiendelee kama wanavyo
hamasishana na kudanganyana tutawadhibiti ili nchi ibaki salama na Watanzania
wema na wapenda amani wabaki salama.
Tungependa kutoa wito kwa
wananchi waendelee kufanya shughuli zao na kufuata maelekezo watakayo kuwa
wanapewa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama maeneo yote nchini sambamba na kutii
sheria za nchi.
Hayo yote yanafanyika ili
Taifa letu liendelee kuwa salama na sisi sote Watanzania wapenda amani
tuendelee kuwa salama wakati wote.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)




0 comments:
Post a Comment