Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza wakati wa kikao chake na Wazalishaji
wadogo wa umeme mkoani Njombe kilichofanyika wilayani Njombe, Mkoa wa Njombe
tarehe 21 Februari 2024. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka
Na Mwandishi wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Wazalishaji
wadogo wa umeme ambapo amewaeleza kuwa, Serikali inawatambua na kuthamini
mchango wao katika uchumi, hivyo wanapaswa kujiamini na kuendelea kubuni miradi
mipya ya kuzalisha umeme ili nchi ipate umeme wa kutosha.
Dkt. Biteko alisema hayo
tarehe 21 Februari 2024 wilayani Njombe mkoani Njombe katika kikao chake na
Wazalishaji Wadogo wa umeme ambacho pamoja na mambo mengine, wazalishaji hao
walieleza changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa kazi zao
pamoja na njia za kuendeleza miradi hiyo.
“Nataka mtambue kuwa, Serikali
haitegemei umeme kutoka vyanzo vikubwa tu kama vile Gesi au mradi wa Julius
Nyerere, bali dhamira yetu ni kuendeleza vyanzo vingine ikiwemo hivi vidogo vya
umeme, hata kama chanzo kinazalisha kilowati moja sisi tunakithamini, hivyo
mnapaswa kujiamini kwani mchango wenu ni mkubwa kwenye Sekta hii.” Alisema Dkt.
Biteko
Dkt. Biteko aliwapongeza
wazalishaji hao wadogo wa umeme kwa ubunifu wao ambao unasaidia katika
kusambaza umeme kwenye maeneo ambayo gridi ya Taifa bado haijafika pamoja na
kuongeza kiwango cha umeme kwenye gridi hiyo kwani wazalishaji wengine
wanaiuzia TANESCO umeme ambao unaingizwa kwenye gridi.
Aliwataka kutoogopa changamoto
na kwamba Serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa namna mbalimbali ikiwemo
kuwapatia nyenzo zinazohitajika.
Ili kutatua changamoto
mbalimbali zilizotajwa na wazalishaji hao wadogo wa umeme ikiwemo suala la
upatikanaji wa vibali na msamaha wa kodi kwa baadhi ya vifaa vinavyotoka nje ya
nchi, Dkt. Biteko ameagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuandaa andiko
litakaloainisha changamoto hizo ili ziweze kufanyiwa kazi na Serikali
kwani Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka biashara ya umeme kuwa rahisi ili
nchi iwe na nishati ya kutosha.
Kwa nyakati tofauti,
wazalishaji hao wadogo wameishukuru Serikali kwa kuwaunga mkono kwenye kazi zao
kupitia TANESCO na REA ambao wanawawezesha kwa namna mbalimbali ikiwemo ushauri
wa kitaalam, fedha na vifaa ambavyo vimewawezesha kuanza kutekeleza miradi
hiyo.
Viongozi mbalimbali
waliohudhuria kikao hicho ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Wabunge wa
Mkoa wa Njombe, Wakuu wa Wilaya na Watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo.
0 comments:
Post a Comment