Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaagiza wataalam kufanya ukarabati wa miundombinu ya umeme kwa wakati ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya umeme ya uhakika.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaagiza wataalam kufanya ukarabati wa miundombinu ya umeme kwa wakati ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya umeme ya uhakika.
Dkt. Biteko amesema tabia ya kutobadilisha au kukarabati miundombinu kwa wakati pale inapoharibika inawakosesha wananchi huduma ya umeme kwa kipindi kirefu.
Amesema hayo tarehe 21 Februari, 2024 wakati wa ziara yake mkoani Njombe ambapo amewasha umeme katika Kijiji cha Ikwavila na Shule ya Sekondari ya Wasichana Njombe iliyoko wilayani Wanging'ombe pamoja na kukagua mindombinu ya uzalishaji umeme na nguzo za umeme katika kiwanda cha TANWAT.
Dkt. Biteko ametoa maagizo hayo baada ya Mbunge wa Wanging'ombe, Mhe. Dkt. Festo Dugange kueleza kuwa, Wilaya hiyo ina changamoto ya radi nyingi zinazosabababisha transfoma kuungua kwa takriban 50 hadi 60 kwa mwaka lakini ubadilishaji wake umekuwa ukichukua muda mrefu na hivyo kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.
"Hili suala la transfoma inaungua halafu inachukua hadi mwezi mmoja kubadiliswa, uzembe huu haukubaliki, Idara ya Manunuzi TANESCO tumeibadilisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kama hii ya uzembe wakati vifaa hivi vinazalishwa kwenye viwanda vya ndani, tunataka watendaji hawa waone shida wanazopata wananchi na kuzitatua, kweli kuna changamoto ya umeme lakini kuna baadhi ya matatizo TANESCO wanaweza kuyamaliza." Amesema Dkt. Biteko
Amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan hataki kero ya umeme iendelee ndio mana utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JHNPP) unaenda kwa kasi na sasa umefikia asilimia 97 na mtambo mmoja umekamilika utakaoingiza megawati 235 kwenye gridi mwezi huu huku mtambo mwingine ukitarajiwa kuingiza megawati nyingine 235 mwezi Machi mwaka huu.
Kuhusu ombi la Mbunge wa Wanging'ombe kupata laini ya umeme inayojitegemea kwani laini ya sasa inatumiwa pia na eneo Lupembe na TANWAT mkoani Njombe na hivyo kufanya umeme wilayani humo kuwa hafifu, ameagiza TANESCO kujenga kituo cha kupoza umeme wilayani humo ili kutengemaza hali ya upatikanaji umeme..
Dkt. Biteko amesema kuwa, Serikali imeamua kwa nia moja kuwaletea maendeleo wananchi kwa kutekeleza miradi katika Sekta zote ikiwemo Miundombinu, Nishati, Afya, Maji na ndio maana wilaya hiyo ya Wanging'ombe imesambaziwa umeme kwenye vijiji vyote 108 na zaidi ya asilimia 56 ya vitongoji wilayani humo vimesambaziwa umeme huku kazi ikiendelea na kwamba shilingi Bilioni 9 zimetengwa kwa ajili ya kusambaza umeme wilayani humo.
Katika hatua nyingine. Dkt.Biteko amewataka wananchi kutoruhusu itikadi za vyama kuwagawanya hasa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu na kusisitiza kuwa watumie uchaguzi huo kuchagua viongozi wanaowaunganisha na kuwaletea maendeleo.
Aidha ameagiza viongozi mbalimbali wa Serikali kujikita kwenye kutatua changamoto.za wananchi na kuwapelekea maendeleo na si kushughulikiana.
Vilevile, Dkt. Biteko ameagiza kuwa, watoto wote wanaopaswa kuripoti mashuleni wafanye hivyo na kuelekeza wasimamizi wa Elimu kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayekwamishwa kuripoti shule kwa sababu ya kigezo cha mavazi kama vile viatu kwani suala la msingi kwa watoto hao ni elimu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Wanging'ombe, Mhe. Dkt. Festo Dugange amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya Afya, Elimu, Nishati na Maji katika wilaya ya Wanging'ombe.
Kuhusu miradi ya umeme vijijini, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwani vijiji vyote108 katika Wilaya ya Wanging'ombe vina umeme na katika vitongoji 523 wilayani humo tayari vijiji 295 vina umeme na kazi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji vingine ikiendelea.
Awali Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini ( REA), Mhandisi Godfrey Chibulunje alisema kuwa, Mkoa wa Njombe umetengewa shilingi biioni 70.44 kusambaza umeme vijijini huku Wangingombe ikipata shilingi bilioni 9.35.
Kuhusu usambazaji umeme vijijini mkoani humo amesema.kuwa katika vijiji 381 tayari vijiji 361 vina umeme sawa na aslimia 94.75
Katika vitongoji amesema kuwa Mkoa una vitongoji 1836 ambapo vitongoji 1148 vina umeme sawa na asilimia 62.5 huku kazi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji vilivyosalia ikiendelea.
Kwa nyakati tofauti viongozi mbalimbali wa Wilaya hiyo wamemshukuru Dkt. Biteko kwa kuwa kiongozi wa kwanza kufika katika kijiji cha Ikwavila na hii ikionesha jinsi anavyofuatilia utekelezaji wa miradi kwa umakini.
0 comments:
Post a Comment