Nafasi Ya Matangazo

February 07, 2024

 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akizungumza na Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Utawala Bungeni jijini Dodoma leo Februari 7,2024 ambapo lengo ilikua ni kusikiliza changamoto wanazokutana nazo kwenye maeneo yao.
Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mhe. Salma Kikwete   akiwasilisha mapendekezo yake katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb)(kulia) na  Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kilichofanyika katika  ukumbi wa Utawala Bungeni jijini Dodoma leo Februari 7,2024 ambapo lengo ilikua ni kusikiliza changamoto  wanazokutana nazo kwenye maeneo yao. Kushoto ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) na Mbunge wa Mtwara, Mhe. Abdallah Chikota (wa pili kutoka kushoto).
Baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii  na taasisi zake wakimsikiliza maoni na mapendekezo ya Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kuhusu changamoto wanazokutana nazo kwenye maeneo yao  katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Utawala Bungeni jijini Dodoma leo Februari 7,2024.
Baadhi ya Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara pamoja na Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb)(hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Utawala Bungeni jijini Dodoma leo Februari 7,2024
*************
Na  Happiness Shayo- Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema Serikali itahakikisha inaendelea kutumia teknolojia ya kisasa kwa kadri inavyowezekana kudhibiti wanyama wakali na waharibifu hususan tembo ili kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.

Ameyasema hayo leo Februari 7,2024 katika kikao chake na Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kilicholenga kusikiliza changamoto  wanazokabiliana nazo wananchi katika  kuthibiti  wanyamapori wakali  na waharibifu katika maeneo yao kilichofanyika leo jijini Dodoma. 

“Katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo tunatumia teknolojia ya Geofencing ambapo tutaweza kupata taarifa endapo tembo  amesogea karibu na uzio uliowekwa na hivyo askari wetu watachukua hatua  za haraka” Mhe. Kairuki amefafanua.

Pia, Waziri Kairuki amesema Serikali imeanza kutumia teknolojia ya kufukuza tembo kwa kutumia kamera za drones ambapo majaribio ya kwanza yamefanyika katika pori la Akiba la Selous.

Kuhusu uzio wa umeme amesema Serikali inaendelea na majaribio kuona kama njia hiyo inafaa au la ambapo kwa sasa majaribio yamefanyika Pori la Akiba la Grumet.

Aidha, amewahakikishia  Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa Serikali inafanya kila liwezekanalo kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yao.

“Niwahakikishie tutakapoweza kukodi helikopta tutafanya hivyo, itakapohitajika kutumia helikopta ya kwetu tutafanya lakini kwa sasa tunaangalia tufanye nini kwa kudhibiti wanyama hao kwa kutumia mikakati ya muda mfupi na ya  muda mrefu”amesisitiza Mhe. Kairuki.

Amesema pia Serikali inafanyia kazi madai ya kifuta jasho na kifuta machozi ambapo mpaka sasa uhakiki umeshafanyika hivyo ufuatiliaji wa fedha unaendelea ili wahusika walipwe.

Kuhusu kutangaza vivutio vya utalii vya ukanda wa kusini, Mhe. Kairuki amesema Serikali itafanya tathmini ya kina kuweza kuviibua, kuvitangaza na kuviendeleza  vivutio vya utalii vya Ukanda wa Kusini hasa Kilwa Kisiwani na maeneo ya fukwe ya Pangani, Mkinga na Mafia.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mhe. Salma Kikwete amesema maeneo mengi ya Mikoa ya Lindi na Mtwara yanakabiliwa na changamoto ya tembo hivyo kuiomba Serikali kutafuta ufumbuzi wa muda mrefu ili kuepuka madhara yanayowapata wananchi hasa kuliwa mazao yao.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb)  Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara, Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)  na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
Posted by MROKI On Wednesday, February 07, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo