Nafasi Ya Matangazo

December 22, 2023

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari kupitia Jukwaa la Wahariri (TEFF) na kusema Wizara yake inakusudia kufanya mageuzi makubwa ya kimfumo wa utendaji katika Sekta ya Ardhi nchini kwa lengo la kuboresha utendaji kazi katika utoaji huduma za sekta ya ardhi nchini.







 Na Eleuteri Mangi, WANMM
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa amesema Wizara yake inakusudia kufanya mageuzi makubwa ya kimfumo wa utendaji katika Sekta ya Ardhi nchini kwa lengo la kuboresha utendaji kazi katika utoaji huduma za sekta ya ardhi nchini.
 
Waziri Silaa amesema hayo Desemba 22, 2023 jijini Dar es salaam wakati wa kikao chake na Wahariri wa vyombo vya Habari kupitia Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhusu siku 100 tangu alipoingia kuhudumo ofisi hiyo alipoteuliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
 
“Wizara inakusudia kufanya mageuzi makubwa ya kimfumo wa utendaji katika Sekta ya Ardhi nchini ambayo yanalenga kuboresha utendaji kazi katika utoaji huduma za sekta ya ardhi” amesema Waziri Silaa.
 
Miongoni mwa maboresho hayo ni Programu ya Kupanga, Kupima, Kumilikisha ardhi (KKK) kwa kushirikisha sekta binafsi na mamlaka za upangaji ambapo katika maboresho hayo yatafanya marekebisho ya utaratibu wa kukopesha fedha kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Viwanja utakaokuwa unatunza fedha na kukopesha fedha kwa ajili ya KKK.
 
Aidha, amesema Wizara inakamilisha maboresho ya mfumo wa TEHAMA ambao utaruhusu huduma na miamala ya sekta kuanza kutolewa kidigitali na mfumo huo utaanza kutumika hivi karibuni kwa kuanza na mikoa ya Arusha, Tanga, Mwanza na Mbeya.
 
Ili kuendana na sayansi na teknolojia, Waziri Silaa amesema kuwa Wizara hiyo imezindua rasmi mfumo wa ARDHI KLINIKI KIGANJANI maalumu wa kupokea na kushughulikia malalamiko yote yatakayowasilishwa kiurahisi kwa kutumia simu ya kiganjani au kompyuta kuwahudumia watanzania katika sekta ya ardhi.
 
Zaidi ya hayo Waziri Silaa amesema kuwa Wizara hiyo inafanya mabadiliko ya kimuundo na ya kiutendaji kwa kuanzisha mikoa maalumu ya ardhi katika maeneo yenye uhitaji mkubwa na kwa kuanzia tumeanza na Mkoa wa Dodoma na Dar es Salaam, maboresho hayo yanaweza kuendelea kufanyika katika mikoa yenye miamala mingi ya ardhi ikiwemo Mkoa wa Mwanza na Pwani
 
Ameongeza kuwa Wizara itadhibiti ujenzi holela wa viwanda na kuelekeza viwanda kujengwa katika maeneo ya kongani za Viwanda na kuongeza maeneo ya kutosha kwa ajili ya Kongani za Viwanda mathalani Kongani ya Viwanda kama Mlandizi na Kwala Chalinze na SinoTan Kibaha.
 
Akimkaribisha Waziri Silaa katika mkutano na Waahariri wa Vyombo vya Habari, Naibu Waziri Mhe. Geophrey Pinda amesema kuwa katika siku 100 za uongozi wake, Waziri ametoa dira na mwelekeo ili wizara iwe na matokeo mazuri ya kuwahudumia watanzania.
 
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa TEF Nevile Meena amesisitiza kuwa Serikali ijihusishe na mipango miji katika maeneo yote nchini badala ya kujihusisha na maeneo ya mijini tu kwa kuwa kwa sasa miji mingi mipya inayofuata barabara imekuwa donda ndugu kwa kuwa haina mipango rasmi kila mtu anajenga kiholela ikiwemo miji ya Kibaha, Picha ya Ndege, Kibaigwa na maeneo mengine nchini.
Posted by MROKI On Friday, December 22, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo