WAZAZI na Walezi wameshauriwa kutoa ushirikiano baada ya kuwapeleka watoto kwenye vituo vya kulea watoto (day care) ili wanapougua ghafla waweze kupatikana na kumuwaisha kwenye kituo cha afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Elimu Mkoa, Mwalimu Abdul Maulid ambapo amesema kuwa, kuna baadhi ya wazazi au walezi wanapompeleka mtoto kwenye kituo hicho hawawafuatilii na mbaya zaidi wanabadilisha namba za simu, inapotokea tatizo hawapatikani, jambo ambalo linaweza kuhatarisha afya ya mtoto katika ukuaji wake.
Amesema kuwa, vituo vya kulea watoto vinachukua watoto wadogo wenye umri kuanzia miaka miwili hadi minne, hivyo basi wanahitaji uangalizi wa karibu ili waweze kukua katika hali ya utimilifu.
Amesema kuwa, hivyo basi kukiwa na ushirikiano wa karibu kati ya mmiliki wa kituo, Mwalimu na mzazi, endapo tatizo inatokeza inakua rahisi kwa watu hao kutafutana na kuangalia namna ya kumsaidia mtoto kabla tatizo hilo halijawa kubwa.
Amesema kuwa, wakati Serikali inatekeleza Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kuanzia umri sifuri hadi miaka minane, inataka wadau mbalimbali kuhakikisha wanatekeleza afua tano za Malezi ambazo ni afya, lishe, ulinzi na usalama, elimu na malezi yenye mwitikio, hivyo basi kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha anashiriki kikamilifu kwenye malezi ya mtoto.
" Kuna baadhi ya wazazi au walezi wakishampeleka mtoto kwenye kituo hawapatikani Tena, hata namba wanazotoa haipatikani, hivyo basi wanapaswa kubadilika na kuweka namba sahihi ambayo itasaidia kupatikana kila wakati ili inapotokea tatizo la ghafla likiwamo la kuugua aweze kutoa ushirikiano, kitendo cha kutopatikana kinasababisha mtoto kuzidiwa,"amesema Mwalimu Maulid.
Ameongeza kuwa, ili kuhakikisha mtoto anakuja katika hali ya utimilifu, Serikali imewapa elimu ya afya walimu wa madarasa ya Awali ili kuwatambua watoto wanaougua ghafla na kuwahi kuwapeleka kituo cha afya kupatiwa matibabu huku wakiendelea kuwatafuta wazazi au walezi wao.
" Walimu wa madarasa ya awali wamepewa elimu ya afya ya mtoto ili inapotokea tatizo waweze kuchukua hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kwenye vituo vya afya kupatiwa matibabu huku wakiendelea kuwatafuta wazazi au walezi.
" Kuna baadhi ya wazazi au walezi ukiwapigia hawapatikani na hata baadhi ya wanaopatikana hawatoi ushirikiano, jambo ambalo linawapa ugumu walimu wa madarasa ya awali kutoa taarifa za watoto," amesema.
Naye mmiliki wa kituo Cha kulea watoto cha Saba Junior kilichopo Manispaa ya Ubungo, Zakaria Kisanga amesema kuwa, wazazi na walezi hawatoi ushirikiano pindi mtoto anapougua ghafla.
" Kuna mtoto aliugua ghafla kwenye kituo chetu, tulipompigia simu mzazi namba haipatikani, tukalazimika kumtafuta dada mlezi ambaye alituambia tumrudishe nyumbani mpaka mzazi wake atakaporudi kwa sababu hana historia ya matibabu ya mtoto, jambo ambalo tuliona linaweza kuhatarisha afya ya mtoto, tukalazimika kumpeleka kituo Cha afya kwanza Ili apatiwe matibabu huku tukiendelea kufanya Mawasiliano nao," amesema Kisanga.
Aliwataka wazazi na walezi hao kuhakikisha kuwa, wanapowapeleka watoto wao kwenye vituo hivyo wanapaswa kufuatilia ili kujua hali ya afya zao, jambo ambalo litakua rahisi kwenye malezi ya mtoto.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bright Jamii Initiative (BJI) Irene Fugara aliwataka wazazi kutoa ushirikiano kwenye malezi ya mtoto kwa sababu utasaidia kuondoka changamoto zinazojitokeza.
" PJT- MMMAM inataka Malezi Jumuishi ya mtoto kuanzia umri sifuri hadi miaka minane, hivyo basi kila mmoja kuanzia mzazi, jamii, wadau hadi Serikali tunapaswa kushirikiana ili kuhakikiaha mtoto anakua katika hali ya utimilifu," amesema Fugara.







0 comments:
Post a Comment