Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt.
Selemani Jafo akielekea kwenye sehemu ya kuwasilishia Hotuba ya Mapitio ya
Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2021/22 na Makadirio ya Mapato na
Matumizi kwa mwaka 2022/23.**********
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo
amewasilisha bungeni Hotuba ya Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa
mwaka 2021/22 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2022/23.
Akiwasilisha
hotuba hiyo leo Aprili 24, 2023, Dkt. Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imekamilisha
taratibu zote za kupata Ithibati ya Kitabu ‘Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar, Chimbuko, Misingi na Maendeleo’ kwa ajili ya
kutumika kama kitabu cha ziada kwa shule za sekondari nchini.
Amesema
kuwa hatua hiyo itasaidia kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu namna Muungano huu
adhimu ulivyoasisiwa pamoja na faida zake ili kuulinda na kuuenzi.
Aidha,
Waziri Jafo amesema kuwa Ofisi imeendelea kuhimiza umuhimu wa wizara, idara na taasisi
zisizo za Muungano kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu, sera,
sheria, utaalamu na wataalamu na hadi kufikia Machi, 2023 vikao 12 vya
ushirikiano vimefanyika baina ya wizara.
Pia, amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea
kuratibu masuala ya Muungano yanayosimamiwa na wizara, taasisi na idara za
Muungano kwa faida ya pande zote mbili za Muungano na kuwa kati ya taasisi 33
za Muungano, 27 zina Ofisi Zanzibar na hivyo kusogeza huduma karibu na
wananchi.
Dkt. Jafo amesema kutokana na hatua hiyo
mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na utambuzi na usajili wa wananchi katika
mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar uliofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho
vya Taifa (NIDA) na kutoa ithibati ya mitaala kwa vyuo vikuu vya Tanzania Bara na
Zanzibar iliyofanywa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni Udahili
wa wanafunzi wa Shahada ya kwanza katika Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania Bara na
Zanzibar kupitia TCU na mafunzo kwa vyuo na shule za sekondari kuhusu Haki za
Binadamu na Utawala Bora kwa pande zote za Muungano. yaliyotolewa na Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Kwa upande wa Hifadhi ya Mazingira Dkt. Jafo
amesema katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Uhifadhi wa
Bonde la Ruaha Mkuu, Ofisi imeshiriki katika utatuzi
wa mgogoro wa ardhi katika Bonde la Mto Ruaha katika eneo la Ihefu ambalo ni
chanzo kikuu cha maji kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Utatuzi wa mgogoro huo ulihusisha Mawaziri
kutoka Wizara nane za Kisekta, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Jumuiya za
Wafugaji, Wawekezaji katika mashamba ya mpunga, wakulima wadogo wa mpunga na
Wananchi wa Wilaya za Mbarali na Chunya.
Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais, itaendelea kuratibu
utekelezaji wa Mpango kazi huo ili kuhifadhi mazingira ya bonde hilo na
ikolojia ya Mto Ruaha Mkuu.
Waziri
Jafo ameomba kuidhinishiwa jumla ya Sh. 54,102,084,000 kwa mwaka wa fedha wa
2023/24.




0 comments:
Post a Comment