Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko ameitaka Kampuni ya Madini ujenzi ya Rocktronic Ltd inayochimba kokoto kuandaa mpango wa huduma kwa jamii inayozunguka mgodi huo kuiwezesha jamii kunufaika na rasilimali madini iliyopo katika maeneo hayo.
Hayo yamebainishwa Januari 6, 2023 alipotembelea machimbo ya kokoto eneo la King'ori katika kampuni ya Rocktronic Ltd wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha.
Dkt. Biteko amesema, mpango huo utasaidia kuwa na malengo ya huduma kwa jamii ili kuleta maendeleo na kuondoa migongano inayoweza kujitokeza siku za baadae na wakazi wa eneo hilo. Amesema mpango huo utasaidia katika kujenga mahusiano mazuri na jamii.
Aidha, ameitaka kampuni hiyo kuandaa taarifa ya upembuzi yakinifu ili kuiwezesha kujua muda wa uhai wa mgodi, kiasi cha mashapo na kiasi kitakacholipwa kwa Serikali.
Akizungumzia utunzaji wa mazingira, Dkt. Biteko ameielekeza kampuni hiyo kuanza kupanda miti katika maeneno ya machimbo ili kuhifadhi mazingira. Ametoa wiki mbili za kuanza kupanda miti na kuitaka kampuni hiyo kuajiri afisa mazingira.
Amesisitiza kampuni hiyo, kuandaa mpango wa uchimbaji ili kuacha kuchimba kwa kuhama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine na kueleza kuwa mpango huo utasaidia kuwa na uchimbaji wenye tija na endelevu.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Rocktronic Ltd Prajesh Chauhan amesema kuwa kampuni hiyo imefanikiwa kutoa ajira ndani ya kata ya Malula kwa wazawa wenye ujuzi na wasio na ujuzi wapatao 118.
Katika hatua nyingine amesema kampuni imechangia shughuli za maendeleo ndani na nje ya kata kwa kutoa vifaa mbalimbali kama vile kokoto, mawe, vifusi na fedha ili kusaidia miradi ya maendeleo ya wananchi katika Sekta ya elimu, afya, maji na barabara za ndani ya vijiji.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha Mhandisi Alphonce Bikulamchi amesema Ofisi ya Madini Arusha itaendelea kushirikiana na wadau wote ikiwemo ofisi ya Mkuu wa Wilaya Arumeru na Mkurugenzi kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija katika shughuli za uchimbaji madini.
Ameongeza kwamba, ofisi itaendelea kutoa elimu juu ya Sheria ya Madini Sura 123 na Kanuni zake pamoja na miongozo mingine ya Serikali ili kuchangia ukuaji wa Sekta ya Madini kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment