Nafasi Ya Matangazo

January 06, 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa taasisi za serikali akiwepo Mkuu wa Mkoa Mstaafu wa Simiyu, David Kafulila.

Rais Samia amemteua David Zacharia Kafulila kuwa Kamishna wa Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP). Kafulila ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mstaafu.

Aidha amemteua Dkt. Ellen Mkondya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa - Muhimbili. Dkt. Mkondya ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Rais Samia, amemteua, Justine Peter Mwandu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Bima la Taifa (NIC). Bw. Mwandu ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Reinsurance (TANRE).  

Katika hatua nyingine Rais Samia, amemteua Prof. Verdiana Grace Masanja kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI). Masanja ni Profesa wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela.

Pia amemteua, Griffin Venance Mwakapeje kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania. Awali, Mwakapeje alikuwa Mkurugenzi, Idara ya Huduma za Kisheria kwa Umma, Wizara ya Katiba na Sheria. Mwakapeje anachukua nafasi ya Bw. Casmir S. Kyuki ambaye atamaliza kipindi chake tarehe 07 Januari, 2023.

Amemteua Bi. Fatma Mohamed Abdallah kuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Puma Energy Tanzania. Bi. Abdallah ni Meneja wa Kampuni ya Puma Energy. Aidha, Bi. Abdallah anachukua nafasi ya Dominic Dhanah ambaye amemaliza muda wake.

Taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus inasema kuwa Teuzi hizo zinaanza mara moja.

Posted by MROKI On Friday, January 06, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo