Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Kozi Fupi ya Kumi na Tatu ya Viongozi kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania, mkoani Dar es Salaam, Agosti 2, 2022.
Baadhi ya washiriki wa Kozi Fupi ya Kumi na Tatu ya Viongozi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua kozi hiyo kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania, mkoani Dar es Salaam, Agosti 2, 2022.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri wanaoshiriki katika Kozi Fupi ya Kumi na Tatu ya Viongozi baada ya kufungua kozi hiyo kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania mkoani Dar es Salaam, Agosti 2, 2022.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax (wa pili kulia) na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania, Meja General Ibrahim Mhona (kushoto) baada ya kufungua Kozi Fupi ya Kumi na Tatu ya Viongozi kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania mkoani Dar es Salaam, Agosti 2, 2022. Wa pili kushoto ni Kansela wa Chuo cha Ulinzi Tanzania, Balozi Matern Lumbanga.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri wanaoshirki katika Kozi Fupi ya Kumi na Tatu ya Viongozi baada ya kufungua kozi hiyo kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania mkoani Dar es Salaam, Agosti 2, 2022.
************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka washiriki wa kozi
fupi ya 13 ya viongozi watambue, wafuate na waisimamie falsafa ya Serikali ya
awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan
iliyojielekeza katika kuwahudumia watanzania.
Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni
kuwaongezea uelewa kuhusu masuala ya ulinzi na stratejia kwa ajili ya kulinda
maslahi mapana ya Taifa katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatarajia kuona mabadiliko
ya kimtazamo, ushauri na maamuzi watakayoyafanya yanapaswa kuakisi
walichokipata kupitia kozi hiyo mara baada ya viongozi hao kurudi kwenye maeneo
yao ya utendaji.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Agosti 2, 2022)
alipofungua kozi fupi ya 13 ya viongozi katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Dar
Es Salaam. Pia kozi hiyo itawaongezea uelewa na ufanisi katika eneo zima la
ulinzi na stratejia kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya Taifa katika
utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatarajia kwamba washiriki
wote, watatumia kikamilifu fursa hiyo adhimu kushiriki kwa umakini na uhodari
wa hali ya juu ili kuongeza uelewa wao wa masuala mtambuka hususan ya kiulinzi,
kiusalama na kistratejia.
Kozi hiyo inahudhuriwa na baadhi ya Mawaziri na Naibu
Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Makatibu
Tawala wa Mikoa na Maafisa Waandamizi kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama na
Taasisi za Kimkakati za Serikali.
“Sisi viongozi wenu tunatarajia kuona kuwa mtakapohitimu
mafunzo haya mtakuwa mmebadilika kimtazamo na hilo halinabudi kujidhihirisha
kwa Wizara na Taasisi mnazotoka kuzungumza lugha moja katika kukabiliana na
changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi yetu.”
“Kwa kufanya hivyo, mtasaidia sana kusukuma maendeleo ya
nchi yetu kwa haraka hasa katika kipindi hiki ambapo Serikali inalenga kukuza
uchumi wa viwanda. Sambamba na hilo, tunapaswa kutambua kwamba changamoto za
sasa ni mtambuka na si rahisi kutatuliwa na Wizara au Taasisi moja moja.”
Akizungumzia Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Waziri Mkuu
ameuagiza uongozi wa chuo hicho uhakikishe
kozi hiyo inakuwa endelevu ili viongozi wengi zaidi wapite hapo na
kufunzwa masuala muhimu yanayohusu ulinzi na usalama kwa nchi yetu.
“Tunahitaji viongozi, watendaji wakuu na maafisa
waandamizi kutoka vyombo vya ulinzi na usalama na ofisi za kimkakati watambue
na kuzingatia maslahi ya nchi, uzalendo, tunu zetu na nidhamu ya kazi kwenye
utendeji wao.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Meja
Jenerali Ibrahim Mhona amesema chuo hicho tangu kianzishwe Septemba 2012
kimepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kutoa kozi ndefu 10 pamoja na kozi fupi
12.
Mkuu huyo wa chuo ameongeza kuwa mafanikio mengine
yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake ni pamoja na kujitangaza na kukubalika
kimataifa ambapo viongozi kutoka mataifa 16 wamehudhuria kozi mbalimbali
zinazotolewa chuoni hapo.
Naye, Kansela wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Balozi Dkt.
Marten Lumbanga amesema mafunzo hayo yanayotolewa kwa viongozi yataleta matokeo
chanya kwa washiriki na kulifanya Taifa lisonge mbele na salama kwani
wataongezewa ueleewa na umakini katika usimamizi madhubuti wa sera kwa usalama
wa nchi.
0 comments:
Post a Comment