Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza na Bw.Muhonja Antony ambaye anafanya kazi za uchomeleaji katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Waziri wa Nishati alifika kisiwani humo ili kukagua hali ya upatikanaji umeme unaozalishwa kwa kutumia mitambo ya umeme Jua.
Nguzo za umeme zilizobeba nyaya ambazo zimesimikwa chini ya ziwa Victoria ili kupeleka umeme wa kiasi cha megawati 10 kwenye kisiwa cha Ukerewe kutokea Bunda –Mara.
***********
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba, amesema kuwa, shilingi 1600 itakuwa bei mpya ya umeme kwa unit katika miradi midogo ya umeme iliyo nje ya Gridi ambayo itaanza kutumika tarehe 1 Agosti, 2022 ili kufanya wananchi kupata umeme wa uhakika na wawekezaji binafsi kuweza kujiendesha na kuwekeza zaidi.
Makamba amesema hayo tarehe 12
Julai 2022 akiwa katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza wakati
alipofika kisiwani humo kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji umeme
wa uhakika.
Maamuzi hayo ya Serikali
yamekuja baada ya wawekezaji binafsi wa miradi midogo ya umeme kutakiwa kuuza
bei ya umeme kwa Shilingi 100 kwa unit gharama ambayo iliwapa changamoto za
kiuendeshaji na hivyo kushindwa kuwapa wananchi huduma ya umeme ya uhakika.
Akiwa kisiwani Ukara, Makamba
alielezwa na wananchi wa kisiwa hicho kuwa, awali walikuwa wakilipa Shilingi
3500 kwa unit na walikuwa wakipata umeme
kwa masaa 24 kwa siku lakini baada ya kutangazwa kwa bei ya umeme ya shilingi 100,
kampuni ya JUMEME inayotoa huduma ya umeme kisiwani humo ilianza kuwapa umeme
kwa masaa Sita tu kwa siku na pia kutakiwa kununua umeme kwa tokeni.
Akitoa ufafanuzi kwa wananchi
kuhusu upangaji wa bei za nishati, alieleza kuwa unapaswa kuhusisha pande zote
mbili ambazo ni Mwekezaji na Serikali hivyo, zoezi la upatikanaji wa bei mpya
ya umeme limekuwa la uwazi na kwamba gharama mpya iliyotajwa haipo juu kama awali ili kutowaumiza wananchi
na pia haitakuwa Shilingi 100 ili kampuni binafsi nazo ziwe na uwezo kufanya
shughuli zake kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Ameeleza kuwa Sera ya Nishati
imetamka wazi kuhusu bei ya nishati inayopangwa na Serikali ikiwemo umeme, gesi
na mafuta, kuwa lazima iendane na gharama za kuzalisha nishati husika.
Pamoja na kutangaza bei hiyo
mpya, Waziri wa Nishati amezitaka kampuni husika kuhakikisha kuwa wanatoa umeme
wa uhakika, wawasilishe mpango wa Biashara serikalini pamoja na kuwa na mkataba
wa huduma kwa mteja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Kampuni ya JUMEME, Bi. Aida Kiangi aliahidi mbele ya wananchi wa UKARA kuwa
kuanzia tarehe 1 Agosti, 2022 umeme kisiwani humo utatolewa kwa masaa 24.
Katika hatua nyingine, Waziri
Makamba ameendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kugawa
mitungi ya gesi 167 ambayo itasambazwa kwa Shule za Serikali za Msingi na
Sekondari kisiwani Ukara pamoja na walimu wa shule hizo ili wawahamasishe
wananchi wengine kutumia nishati safi.
Awali, Waziri wa Nishati alikagua
vituo vidogo vya mafuta wilayani Bunda, Mkoa wa Mara katika Kijiji cha Guta B
na Kibara ikiwa ni mkakati wake wa kupeleka vituo vya mafuta hadi vijijini ili
wananchi wapate Nishati safi na katika mazingira salama ambapo katika Mwaka wa
Fedha 2022/2023 Serikali imetenga Shilingi Bilioni 2 ili kutoa mikopo kwa
wananchi wanaotaka kuwekeza katika ujenzi wa vituo hivyo vijijini.
Akiwa safarini kuelekea wilayani Ukerewe Waziri Makamba alikagua nyaya za umeme zinazopita chini ya Ziwa Victoria ambazo zinapeleka umeme wa kiasi cha megawati 10 wilayani humo zikitokea Kisorya wilayani Bunda.
0 comments:
Post a Comment