Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua
Mkoani Tabora Jerry Mwaga
Na Lucas Raphael,Tabora
HALMASHAURI ya Wilaya ya
Kaliua Mkoani Tabora imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 848.9 za
marejesho ya mikopo itokanayo na asilimia 10 ya mapato ya ndani iliyotolewa na
halmashauri hiyo kwa vikundi zaidi ya 70.
Hayo yamebainishwa jana na
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga alipokuwa akiongea na
mwandishi wa gazeti hili aliyetaka kujua mafanikio ya utekelezwaji agizo la Waziri
Mkuu kwa halmashauri zote kuhakikisha fedha za mikopo zinazotolewa
zinarejeshwa.
Alisema licha ya kuendelea
kutekeleza agizo la serikali la kuwezesha vikundi vyote vya akinamama, vijana
na watu wenye ulemavu mikopo nafauu isiyo na riba, pia wameweka mkakati wa
kufuatilia urejeshwaji mikopo hiyo ili vikundi vingi zaidi vinufaike.
Alibainisha kuwa hadi sasa
jumla ya shilingi 848, 922, 050.
zimesharejeshwa ambapo vikundi vya wanawake pekee vimerejesha kiasi cha
shilingi 534, 313, 050. vijana wamerejesha
shilingi 300,425,000. na watu wenye
ulemavu shilingi 14,184,000.
Mwaga alifafanua kuwa zoezi la
ukusanyaji marejesho ya mikopo hiyo linaendelea katika vikundi vyote na sasa
imebakia kiasi cha sh milion 647.2 kati
ya zaidi ya shilingi bilion 1.5 zilizokopeshwa na halmashauri hiyo.
Aliongeza kuwa fedha
zinazorejeshwa mbali na kuendelea kutolewa kwa vikundi vingine pia zimekuwa
zikisaidia kutekeleza shughuli nyingine za kimaendeleo ikiwemo kukamilisha
miradi inayokwama.
‘Nimeshaelekeza timu ya mapato
kwa kushirikiana na Maofisa Maendeleo ya Jamii na Watendaji kuongeza kasi ya
ufuatiliaji ili vikundi vyote vikamilishe marejesho ya mikopo yao kwa wakati’,
alisema.
Mwaga aliongeza kuwa mbali na
kuendelea kutoa mikopo hiyo halmashauri ina mkakati wa kuanzisha kiwanda cha
kuchakata mazao ya nyuki kupitia fedha hizo na zile za mapato ya ndani, hivyo
akavitaka vikundi vyote kurejesha kwa wakati.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo
Jafael Lufungija alibainisha kuwa ili kufanikisha mkakati huo wamepeleka timu
ya watalamu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi kujifunza namna
ya kuanzisha na kuendesha kiwanda hicho.
Alibainisha changamoto iliyopo
kuwa ni baadhi ya vikundi kutorejesha mikopo yao kwa wakati ila akasisitiza
kuwa wataendelea kuvifuatilia ili virejeshe fedha hizo huku akiongeza kuwa
vitakavyokaidi vitafikishwa mahakamani.
0 comments:
Post a Comment