KATIBU MKUU wa Jumuiya ya vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)Ndg Kenani Kihongosi(katikati) akiwa na vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati akizindua rasmi kampeni ya uhamasishaji wananchi hususani vijana kwaajili ya kujiandaa na ushiriki wa sensa ya watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23,2022.Na Kevin Lameck
KATIBU MKUU wa Jumuiya ya vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)Ndg Kenani Kihongosi amefungua rasmi kampeni ya uhamasishaji wananchi hususani vijana kwaajili ya kujiandaa na ushiriki wa sensa ya watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.
Tukio hilo limefanyika leo wilayani Temeke mkoani Dar es salaam katika viwanja vya Mwembeyanga huku likipambwa na elimu mbalimbali kutoka kwa maafisa na waratibu wa Sensa sambamba na burudani za wasanii mbalimbali waliotumia sanaa zao kuwahamasisha vijana kujitokeza kuhesabiwa na kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa zoezi hilo.
Kulingana na Kenani Kihongosi, Katibu Mkuu wa UVCCM,kampeni hiyo ya hamasa na elimu kuhusu Sensa 2022 inatarajiwa kufanyika nchi nzima chini ya uratibu wa jumuiya ya vijana wa Chama Cha Mapinduzi nchini Tanzania.
Akizungumza na mamia ya vijana katika viwanja vya Mwembeyanga, Katibu Mkuu Kenani amesema Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini, kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum.
Kwa maana nyingine, sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi.
Amesema Takwimu hizi za msingi ndiyo zinazoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano, watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo.
Katibu Mkuu wa UVCCM Kenani Kihongosi amesema umuhimu wa zoezi hilo ni kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa.
Aidha Kihongosi amesema taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya na serikali kuu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali za taifa.
Kulingana na makamishna wa sensa,miongoni mwa maswali yatakayoulizwa yatahusu:-Taarifa za kidemografia (umri, jinsi, uhusiano, hali ya ndoa, uraia, n.k.); Maswali yanayohusu ulemavu; Taarifa za Elimu; Maswali ya uhamaji, pamoja na taarifa za Watanzania wanaoishi nje ya nchi sambamba na Taarifa za Uzazi na Vifo vilivyotokea ndani ya kaya
0 comments:
Post a Comment