Akifungua Mafunzo ya siku tatu
jijini hapa yaliyokutanisha washiriki 162, Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Mh.
Balizi Omari Ramadhani Mapuri alisema, wasimamizi hao wa uchaguzi katika kanda
ya Kati wanatakiwa kuzingatia maadili wanapofanya kazi hiyo.
Alisema uchaguzi ni mchakato
unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa
akisisitiza kwamba hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi mzuri wenye
ufanisi usio na malalamiko.
Balozi Mapuri alisema wasimamizi
hao, katika mkutano huo wa siku tatu (3) wanatakiwa kubadilishana uzoefu,
kujadili namna bora ya kufanikisha uchaguzi, lakini pia kujadili namna bora ya
kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika hatua mbalimbali za
uchaguzi.
Aidha Balozi Mapuri, aliwataka
wasimamizi hao kufanya kazi kwa kufuata maadili kwa kuzingatia Sheria, Kanuni
pamoja na maagizo na maelekezo yanayotolewa na Tume ya Uchaguzi.
“Mnatakiwa kutumia mkutano huu,
kubadilisha uzoefu na kufanya kazi kwa kufuata maadili kwa kuzingatia sheria,
kanuni na maelekezo pamoja na maagizo ya Tume ya uchaguzi,” alisema.
Balozi Mapuri alisema wasimamizi
hao wameaminiwa na kuteuliwa na Tume katika nafasi hizo za usimamizi wa
uchaguzi kwa kuwa wana uwezo wa kufanya kazi hiyo hivyo wanatakiwa wajiamini na
kujitambua.
Alitoa mwito kwa wasimamizi hao
kuhakikisha kuwa wanayaelewa vema maeneo yao ya kazi kijiografia na kuhakikisha
kwamba wanawatumia vizuri wasaidizi walio chini yao katika maeneo yao ili kutoa
matokeo bora.
Pia aliwataka wasimamizi hao
kujua miundombinu mbalimbali ya kufika kwenye vituo vya kupigia kura katika
majimbo wanayosimamia uchaguzi.
Balozi Mapuri aliwataka
washirikishane na vyama vya siasa pamoja na wadau wengine wa uchaguzi katika
mstakabali mzima wa uchaguzi ili kuongeza uwazi katika uchaguzi na hivyo kuleta
ufanisi.
Kati ya washiriki wa mkutano huo,
wasimamizi wa uchaguzi wapo 24,
wasimamizi wasaidizi uchaguzi katika majimbo wapo 87, maafisa
uchaguzi 24, waratibu wa uchaguzi watatu
na maafisa ugavi 24 ambapo kati yao 55 wanatoka mkoa wa Dodoma, Morogoro 61 na
Singida 46.
Katika kwenda kutekeleza
kikamilifu majukumu yao usimamizi hao katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba
28, mwaka huu, walikula viapo viwili moja cha kujitoa katika vyama vya siasa na
nyingine ya kutunza siri za uchaguzi wanaposimamia uchaguzi.
Kiapo hicho cha utii kiliongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi Wilaya ya Dodoma, Mary Senapee ambaye aliwataka washirikishi hao kusaini baada ya kuapa kwani wakikiuka maadili ya uchaguzi ndicho kitakacho wafunga.
0 comments:
Post a Comment