Nafasi Ya Matangazo

December 06, 2019

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa anafuatilia mkutano wa Baraza la Mawaziri wa nchi za Afrika,Carribean na Pacific (ACP).
Nyuma ya Prof. Kabudi ni Balozi wa Tanzania Nchini Kenya Balozi Pindi Chana akifuatiwa na Balozi wa Tanzania Nchini Ubelgiji na katika Jumuiya ya Ulaya Balozi Jestas Nyamanga
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa anajadiliana jambo na Balozi wa Tanzania Nchini Ubelgiji na katika Jumuiya ya Ulaya Balozi Jestas Nyamanga (aliyesimama) akifuatiwa na Balozi wa Tanzania Nchini Kenya Balozi Pindi Chana pamoja na baadhi ya maafisa wa Ubalozi na wa Wizara ya Mambo ya NJe na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (KICC) Nairobi Kenya.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwasilisha hoja ya Tanzania katika Mkutano wa 110 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi za Afrika,Carribean na Pacific (ACP) katika ushirikiano na Jumuiya ya Ulaya unaofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (KICC) Nairobi, Kenya. Nyuma ya Prof. Kabudi ni Balozi wa Tanzania Nchini Ubelgiji na Jumuiya ya Ulaya Balozi Jestas Nyamanga.
**************
Tanzania imetoa mapendekezo makuu matatu na yamekubaliwa katika kikao cha mashauriano baina ya Mawaziri wa Baraza la Nchi za Afrika,Carribean na Pacific kilichoanza leo jijini Nairobi, Kenya. 

Mapendekezo hayo ya Tanzania yametolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Prof. Palamagamba John Kabudi katika Mkutano wa 110 wa Baraza la mawaziri wa wa Nchi za Afrika,Carribean na Pacific katika ushirikiano na Jumuiya ya Ulaya ambao utafuatiwa na Mkutano wa tisa wa wakuu wa Nchi na Serikali katika jiji la Nairobi Nchini Kenya na kuongeza kuwa Tanzania imetoa mapendekezo hayo ili kutodhoofisha umoja wa ACP hususani katika kipindi hiki ambacho nchi hizo ziko katika majadiliano ya kina na Jumuiya ya ulaya kuhusu mkataba mpya wa ushirikiano baada ya mkataba wa sasa unaofikia ukomo Februari mwakani.

Mapendekezo ya Tanzania yaliyokubaliwa na kuingizwa kama sehemu ya maazimio ya Baraza la Mawaziri ni hoja ya kutokuruhusu wanachama washiriki nje ya wanachama wa ACP, (Associate members),kutoingiza wanachama watazamaji kutoka katika makundi yaliyoganyika kutoka katika serikali zao na ambazo hazitambuliwi na mamlaka za serikali za nchi wanachama pamoja na kutaka majadiliano ya kisiasa baina ya nchi za ACP na Umoja wa Ulaya kuendelea kusalia katika mamlaka za serikali za Nchi za Afrika,Carribean na Pacific badala ya kuyaamishia katika Bunge la ACP.

Ameitaja sababu nyingine kuwa ni kuepuka mivutano isiyo na tija kati ya Nchi za Afrika,Carribean na Pacific na Nchi za Jumuiya ya Ulaya hususani katika nyakati ambazo nchi hizo zinahitaji mshikamano mkubwa zikiwa zinapita katika kipindi muhimu cha kujenga uchumi na ustawi wa jamii ya nchi zao na pia kujenga wigo wa kuaminiana baina ya Nchi wanachama.

Ameongeza kuwa majadiliano baina ya Nchi wanachama wa ACP ni muhimu ili kupitia upya mkataba wa George Town,mkataba ambao ndiyo ulianzisha Kundi la ACP na kusainiwa katika jiji la Goergetown nchini Guyana mwaka 1975. 

Nchi za ACP zimekubaliana kufanya mabadiliko makubwa ya Mkataba huo ili kujenga Umoja wa ACP unaoendana na mabadiliko ambayo yamejitokeza ulimwenguni na masuala mbalimbali ya Kimataifa ambayo yanahitaji mtazamo mpya.

Prof. Kabudi amesema katika muktadha huo wa majadiliano, Tanzania imetoa mapendkezo hayo matatu ambayo yote yamekubaliwa na kuungwa mkono na nchi zote 79 wananchama wa ACP jambo linaloonesha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaheshimika sana katika masuala ya kimataifa.

Akizungumzia juu ya faida ya Mkutano huo wa Nchi za Afrika,Carribean na Pacific , Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji ambaye pia anaiwakilisha Tanzania katika Jumuiya ya Ulaya Balozi Jestas Abuok Nyamanga amesema kuwa mkutano huo unatumika kama kutoa fursa kwa nchi 79 wanachama wa ACP kutathmini changamoto mbalimbali zinazokabili nchi hizo, kuweka mikakati ya pamoja na kuwa na sauti ya pamoja katika kusimamia utekelezaji wa mikakati hiyo na katika majadiliano na Jumuiya ya Ulaya. 

Alisema kuwa miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa na kuwekewa mikakati ya pamoja ni pamoja na masuala yanayohusu uwekezaji, viwanda na biashara; uongezaji wa mnyororo wa thamani katika mazao ya kilimo, kuongeza uwezo na wigo wa ukusanyaji wa kodi. 

Mkutano huo pia unajadili namna ya kuwaongezea uwezo wafanyabiashara wadogo,kuongeza ubunifu na matumizi sahihi ya teknolojia na kukabiliana na mabadiliko ya tabiachi. Masuala yote hayo ni moja ya kipaumbele cha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu hii ya tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli.

Amehitimisha kwa kusema katika mkutano huu Katibu Mkuu wa ACP anatarajiwa kuchaguliwa ili kuweka mfumo mpya wa kiuongozi utakaosaidia wanachama wa ACP kupita katika ushirikiano kwa miaka mingine ijayo katika ushirikiano baina ya nchi za Afrika,Carribean na Pacific na Jumuiya ya Ulaya.
Posted by MROKI On Friday, December 06, 2019 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo