Muonekano wa sehemu ya jengo la Kambi ya Kijiji cha Njia nne Wilaya ya Kilwa
Meneja Mawasiliano na Mahusiano wa TPDC Bi. Marie Msellemu akikabidhi hati ya makabidhiano ya Kambi Namba 8 kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa Dr. Khalfan Ilekizemba.
Hati ya Makabidhiano ya Kambi Namba 8 kati ya TPDC na Kijiji cha Njia nne, Wilayani Kilwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Daktari Khalfani akiwa na jopo la wadau wa maendeleo katika hafla ya kukabidhi kambi.
*****************
Na Mwandishi Wetu.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendelea kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii kwa Vijiji na Mitaa inayoguswa na miundombinu ya bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es salaam. Katika kufikia azma hii TPDC imekabidhi kambi Namba 8 kwa kijiji cha Njia nne Wilayani Kilwa ili Kijiji kiweze kupanga matumizi sahihi ya Kambi hiyo.
Kukabidhiwa kwa majengo ya Kambi hayo kunatokana na kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya bomba la gesi asilia kutoka Madimba-Mtwara na Songosongo hadi Dar es Salaam, hivyo kufanya majengo hayo kutotumika tena kwa shughuli za ujenzi.
Akikabidhi rasmi kambi hiyo kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Njia nne hivi karibuni, Meneja Mawasiliano na Mahusiano wa TPDC Bi. Marie Msellemu alisema kuwa “Mikoa ya Lindi na Mtwara ni wadau wakubwa katika ustawi wa miundomibinu ya bomba la gesi asilia na tumekuwa tukishirikiana katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo na ya kijamii ikiwemo afya, michezo, utawala bora na maji lengo ikiwa ni kudumisha mahusiano mema na kuboresha huduma muhimu za kijamii, na hivyo kuwataka wananchi wa mikoa hii ya kusini kushirikiana na TPDC katika kuilinda miundombinu ya gesi asilia na kwa pamoja kuboresha huduma za jamii’’.
Katika hafla ya kukabidhi Kambi hiyo, Kaimu Mkurugezi wa Wilaya ya Kilwa Dr. Khalfani alitoa shukrani za dhati kwa TPDC kwa kuwa mdau mkubwa na wa karibu katika shughuli mbalimbali za maendeleo Wilayani Kilwa hasa katika kuboresha sekta ya elimu na afya.
‘Tunalishukuru Shirika la TPDC kwa kutupatia kambi hii ambayo itasaidia Halmashauri na Kijiji kupanga matumizi sahihi katika nyanja ya afya, Shule au nyumba za watumishi wa umma’’. Pia, alisema kuwa tayari kambi hiyo yenye uwezo wa kuchukua kaya/familia 25 imeshaanza kutumika kwa kusaidia makazi kwa waajiriwa wapya wa Halmashauri.
Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Tingi Bw. Bayani Saidi Mtenda katika kutoa shukrani zake alisema sambamba na TPDC kutoa Kambi hiyo , Serikali ya Kijjji na wananchi kwa ujumla wanawajibu wa kuilinda na kuhakikisha usafi wa mazingira unaimarishwa ili iweze kudumu na kuwa na tija kwa manufaa ya Kijiji.
Aidha, alisema kwamba Mkutano Mkuu wa Halmashauri ya Kijiji ndiyo utakaoamua na kupanga matumizi ya kambi hiyo ikiwa ni pamoja na kupanga Kodi/tozo kwa watakaobahatika kuyatumia majengo ya Kambi hiyo.
Bayana alitoa wito kwa TPDC na wadau wengine wa maendeleo kuendelea kusaidia shughuli za maendeleo kijijini hapo kwani Kijiji kinachangamoto kubwa hasa katika Sekta ya elimu na kuweka bayana mapungufu ya vyumba vya madarasa hali inayopelekea wanafunzi kusomea chini ya miti.
0 comments:
Post a Comment