Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za
rambirambi Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Mhe. Benjamin William Mkapa
(Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu) kufuatia kifo cha Makamu Mkuu wa chuo hicho
Prof. Egid Beatus Mubofu kilichotokea leo tarehe 18 Desemba, 2018 huko
Pretoria, Afrika Kusini.
Prof. Mubofu alipelekwa
Jijini Pretoria kwa matibabu zaidi akitokea Taasisi ya Tiba ya Mifupa katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) alikokuwa akipatiwa matibabu ya kiharusi.
Mhe. Rais Magufuli
amemuomba Mhe. Mkapa kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya Marehemu
Prof. Mubofu, Wahadhiri na wafanyakazi wa UDOM, Wanafunzi wote wa UDOM, Jumuiya
na taasisi zote ambazo Prof.
Mubofu alifanya kazi na
wote walioguswa na msiba huu. “Nimesikitishwa sana na kifo cha Prof. Mubofu,
nitamkumbuka kwa uchapakazi wake,
ubunifu, uadilifu na uaminifu mkubwa aliouonesha katika utumishi wake kwa Taifa
ikiwemo kazi nzuri aliyoifanya katika Shirika la Viwango la Taifa (TBS) akiwa
Mkurugenzi Mkuu, kabla ya kuteuliwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha UDOM”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli
ameiombea familia ya Marehemu Prof. Mubofu kuwa na moyo wa subira na uvumilivu
na amemuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi,
Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Desemba, 2018
0 comments:
Post a Comment