Mwandishi Wetu
KISUKARI ni ugonjwa unaoonyesha viwango vikubwa vya glukosi katika damu. Sababu yake ni uhaba wa homoni ya insulini mwilini au upungufu wa uwezo wa mwili wa kukubali insulini.
Kuna watu wanaozaliwa wakiwa hawana insulin hiyo inayochochea matumizi ya sukari, hivyo kuwa na kisukari cha utotoni na kuna wanaokipata kutokana na mwenendo wa tabia za maisha.
Vile vile, kuna wanawake wanaokipata wakati wakiwa wana mimba lakini baada ya kujifungua hupana na mwili wao unarejea katika hali ya kawaida.
Kwa ujumla ugonjwa wa kisukari hutokana na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kuliko inavyotakiwa au kuna mkwamo wa matumizi mwilini. Sukari kwenye damu ikizidi viwango vya kawaida kwa muda mrefu husababisha madhara mengi mwilini.
Chama cha Ugonjwa wa Kisukari (TDA) katika taarifa yake juu ya “nini ufahamu kuhusu ugonjwa wa kisukari’ kinasema sukari mwilini hutokana na vyakula pamoja na vinywaji ambavyo mtu anavitumia kila siku na kazi yake kubwa ni kuupa mwili nguvu.
Athari za ugonjwa wa kisukari
Ugonjwa wa kisukari unasababisha athari nyingi mwilini. Miongoni ni pamoja na magonjwa ya moyo kuwa zaidi ya mara mbili zaidi ya watu wasio na ugonjwa huo. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HAYA.
Matatizo mengine ni shinikizo la damu, kiharusi, kuharibika mishipa ya damu na ile ya fahamu kiasi cha kusababisha ganzi, vidonda na hata gangirini ya miguu. Takwimu zinaonyesha kwamba ugonjwa wa kisukari ni moja ya sababu za watu wengi kukatwa miguu.
Ugonjwa wa kisukari pia husababisha kuharibika kwa figo na kuzifanya kushindwa kufanya kazi. Pia husababisha matatizo ya macho na upofu.
Madhara mengine ni kupungua kwa kinga ya mwili na kuuweka mwili katika hatari ya maambukizi ya ngozi, fizi, njia ya mkojo, uke na kifua kikuu. Vile vile unaweza kusababisha kupungua nguvu za kiume, utendaji wa kazi na kuathiri uchumi.
Dalili za Kisukari
Zipo dalili nyingi lakini miongoni ni kuhisi kiu mara kwa mara, kwenda haja ndogo mara kwa mara, kuwa dhaifu, uchovu kila wakati, kupungua uzito au kukonda.
Dalili nyingine ni kusikia njaa kila wakati, wanawake huwashwa sehemu za siri, kutoona vizuri, kupungua nguvu za kiume, ganzi, kuhisi kuchomwachomwa, miguu kuoza, vidonda na majeraha kutopona haraka na majipu mwilini.
Namna ya kujikinga na kisukari
Mwenyekiti wa TDA, Profesa Andrew Swai anasema mtu anaweza kujikinga na ugonjwa wa kisukari kwa kupunguza unene kwani hupunguza uwezo wa mwili kutumia sukari.
“Uzito wako usizidi urefu mara urefu mara 25. Kwa mfano mtu mwenye urefu wa mita 1.63 uzito unatakiwa usizidi 1.63 x 1.63 x 25 ambayo ni sawa na kilo 66. Urefu uwe kwa mita na uzito uwe kwa kilo.
Njia nyingine, anasema ni kujishughulisha mwili kwa kufanya chocchote kitakachokufanya utoke jasho au moyo kwenda mbio kwa angalau nusu saa kila siku, hata kama sii mnene.
Kujishughulisha ni kufanya jambo lolote la kutumia misuli mwilini, kwa mfano kutembea, kukuimbia, kufanya kazi za nyumbani, kulima, michezo mbalimbali na kucheza dansi.
Kujishughulisha ni muhimu sana kwa matumizi ya sukari mwilini na afya kwa ujumla. Kukaa kwa muda mrefu bila kujishughulisha nako sii vizuri, inatakiwa usikae zaidi ya saa moja bila kujishughulisha, kwa angalau dakika mbili au tatu.
Njia nyingine ni kupunguza matumizi ya pombe au kuacha kabisa, kutotumia sigara au aina yoyote ya tumbaku na kuepuka misongo ya mawazo. Msongo wa mawazo ni kisababishi kikubwa cha kisukari na sukari kuzidi kuwa juu kwa walio na kisukari.
Tunaweza kuepuka misongo mingi kwa kuwa wakweli kuhusu mahitaji yetu ya lazima, uwezo wetu na muda tulionao. Tuna haja ya kuamua ni kipi tuwaachie wengine au kushirikiana kwani mtu mmoja hawezi yote.
Njia ya mwisho lakini iliyo na umuhimu mkubwa ni kula chakula inavyotakiwa. Sehemu kadhaa za mwili hufanya kazi muda wote tangu kuzaliwa hadi kufa bila kupumzika. Viungo hivyo ni kama ubongo, mapafu, moyo na figo.
Hivyo mwili unahitaji sukari kila dakika. Kuwezesha hili, vyakula vyote vimeumbwa vigumu; sio vya kumiminika, ili vitulie tumboni.
Tumbo linavisaga na kuviachia kidogo kidogo kadiri mwili unavyohitaji, kitu ambacho hakitawezekana ikiwa chakula tayari ni cha kumiminika.
Maziwa ya mama ni ya kumiminika ili yapite kwenye matiti lakini yakifika tumboni mwa mtoto mara hugandishwa ili nayo yatulie na tumbo lifanye kazi yake. Hatima ya vyakula vyote vyenye wanga tumboni na kwenye utumbo ni sukari.
Vimeumbwa vile ili sukari ipatikane polepole kwa taratibu za mmengenyo wa vyakula mwilini. Magamba yameingizwa kwenye nafaka na mboga mboga pia kwa ajili hiyo.
Sukari ikiingia kwenye mwili kwa wingi huharibu sehemu nyingi za mwili. Hivyo inashauriwa tusiongeze sukari kwenye vyakula. Matumizi ya sukari yasizidi vijiko vya chai vitano kwa mtu kwa siku. Tusikoboe nafaka na tule matunda yalivyo badala ya kutengeneza juisi.
Mlo wenye mboga mboga kwa wingi huongeza magamba kwenye chakula na kupunguza kasi ya sukari kuingia mwilini.
Nani anaweza kuugua kisukari
TDA inasema kwamba tafiti mbalimbali zilizofanywa hapa nchini na duniani zimebaini kuwa mtu yeyote anaweza kupata ugonjwa wa kisukari.
TDA inaeleza kuwa tafiti zilizofanywa hapa nchini zimebaini kwamba Watanzania tisa kwa kila 100 wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wanaugua ugonjwa wa kisukari.
Mbaya zaidi, TDA inaeleza kuwa kati ya hao tisa ni wawili tu ambao wanajijua kuwa wanaugua kisukari. Wale wasiojijua huendelea kusishi na kisukari kwa muda mrefu na hugunduliwa baada ya ugonjwa kusababisha madhara makubwa mwilini yasiyofichika.
Hivyo watu wote wenye miaka 45 na kuendelea wanashauriwa kupima afya angalau mara moja kila mwaka ili kugundua kama wana kisukari au magonjwa mengine ambayo mwanzoni hayana dalili, kama vile msukomo wa juu wa damu, magonjwa ya moyo, na hata saratani.
Hadi sasa, TDA inasema ugonjwa wa kisukari hauna dawa ila mtu mwenye kisukari anaweza kuishi maisha marefu kama watu wengine ikiwa atafuata ushauri wa wataalamu jinsi ya kuuthibiti ugonjwa.
Makala haya yameandaliwa na:
Jukwaa la Waandishi wa Habari Wanaopambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TJNCDF), S L P 13695, Dar es Salaam. Baruapepe: tjncdf@gmail.com.
0 comments:
Post a Comment