Mwandishi Wetu
AKIWA amelazwa katika Taasisi ya Taifa ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), iliyopo jijini Dar es Salaam anaeleza kuwa afya yake imedhoofu sana ukilinganisha na hali halisi aliyokuwa nayo miaka mitatu iliyopita.
Crisent Bagara (62) anasema baada ya uchunguzi madaktari wa ORCI wanasema anasumbuliwa na saratani ya koo iliyotokana na uvutaji wa sigara.
Bagara anasema anahisi kushiwa nguvu, hawezi kumeza chakula na familia yake kwa sasa imeathirika kiuchumi kutokana na gharama kubwa za matibabu ya saratani.
Bagara ambaye kwa sasa anapata tiba ya mionzi anasema anajuta kujiingiza kwenye matumizi ya sigara kwa kuwa licha ya kumuathiri kiafya kwa muda mrefu imemrejesha kwenye umaskini.
“Nilikuwa mkulima wa mahindi, maharagwe, alizeti na mazao mbalimbali eneo la Oldian, wilaya ya Karatu, mkoani Arusha. Nilipata fedha nyingi, nimesomesha watoto hadi sasa wanajitegemea na sikuwahi kupata shida ya kifedha,” anasema.
Tangu ameanza kuumwa miaka mine iliyopita anasema kidogokidogo kasi yake ya kujiingiza kwenye kilimo ilipungua. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HAYA.
Kwa sasa anasema mkewe pamoja na watoto wanatumia muda mrefu kumhudumia na raslimali nyingi za fedha zinaingizwa katika matibabu na gharama za kusafiri na kutumia huko na kule wanakompeleka kumtibia.
“Nawahurumia sana kwa jinsi wanavyohangaika kunihudumia na fedha zimewaishia. Najuta kuvuta sigara. Kwa kweli sigara ni mbaya,” anasema Bagara akifafanua:
“Naomba serikali ipige marufuku sigara na kilimo cha tumbaku. Nashauri wakulima wawe na mazao mbadala.”
Akielezea historia yake, anasema alianza kuvuta sigara akiwa na umri wa miaka 20 na alikuwa na uwezo wa kumaliza pakiti tatu kwa siku.
Bagara anahudumiwa na mtoto wake wa pili wa kiume, Aveline amabaye anasema baba yake amelazwa kwenye hospitali hiyo kwa miezi mitatu.
“Baba hawezi kula. Akitumia hata uji mwembamba anataapika. Anachotumia ni dripu la lishe ambalo hapa hospitali halipatikani inabidi kulinunua.
“Gharama yake ni kubwa linauzwa sh. 300,000 na analitumia kwa siku tatu. Kwa wiki tatu atatumia saba. Ina maana zinahitajika sh. milioni 2.1. Ukijumuisha gharama zote ni karibu milioni tatu.”
Anasema licha ya kwamba matibabu ya saratani hutolewa na serikali bure, wastani wa matumizi ya miezi mitatu atakayodumu ni sh. milioni 12.
Anasema hizi ni gharama kubwa ukilinganisha na uwezo wa familia hiyo ambayo kwa sasa karibu shughuli nyingi za kuzalisha zimesimama nguvu ikielekezwa kwenye matibabu.
Anaelezea baba yake alianza kwa kupata kikohozi cha kawaida mwaka 2013 na akawa anahudumiwa katika zahanati eneo la Oldian.
Alitumia dawa mbalimbali hata za kienyeji lakini hakupona na badala yake akaanza kukohoa damu.
“Hii iliashiria hali ya baba ni mbaya tukahisi ni TB. Tulimpeleka kwa daktari maarufu Frenc na alipomchunguza akabaini ana saratani ya koo. Akatushauri tumpeleke hospitali ya Selian.”
Baada ya matibabu ya muda mfupi Seliana anasema alipewa rufaa akatibiwe Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Anasema yeye havuti sigara lakini kaka yake anatumia lakini aliacha baada ya kuona jinsi baba yao anateseka.
Dalili za saratani ya koo
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk Crispin Kahesa anasema mgonjwa mwenye saratani ya koo katika hatua za awali anaweza asionyeshe dalili.
Hata hivyo, kadiri saratani inavyozidi kukua na kuenea, mgonjwa anaweza kuanza kuona dalili.
“Siku za mwanzo mgonjwa anaweza kushindwa kumeza chakula kigumu kisha cha majimaji na baadaye akashindwa kumeza hata mate,” anasema.
Anaongeza kuwa maumivu wakati wa kumeza chakula hasa chakula kigumu, maumivu kwenye kifua au mgongoni, kupungua uzito, kiungulia, sauti ya mkwaruzo au kikohozi kikavu cha zaidi ya wiki mbili," anasema.
Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania, Lutgard Kagaruki anasema kuna haja ya kudhiti matumizi ya tumbaku nchini kwa kupiga marufuku matangazo, promosheni na ufadhili wa tumbaku nchini.
"Katika hili, mwendelezo wa matangazo, promosheni na ufadhili wa bidhaa za tumbaku Tanzania umesababisha ongezeko kubwa la matumizi ya tumbaku miongoni mwa vijana,” anasema Kagaruki.
Anasema hayo yanatokana na utafiti uliyofanywa mwaka 2008 na Global Youth Tobacco Survey na kubaini kuwa asilimia 10.6 ya wanafunzi nchini wanatumia bidhaa zinazotokana na tumbaku.
Anasema utafiti uliofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mwaka 2010 ulionyesha kuwa zaidi ya asilimia 32 ya saratani zote za wagonjwa waliowatibu kilichosabnabisha ni matumizi ya tumbaku.
Ili kutibu saratani hiyo, alisema Serikali inatumia zaidi ya dola za Marekani 40 milioni (Sh6.4 tirioni) kuhudumia wagonjwa.
Anayataja matatizo mengine yanayohusishwa na matumizi ya tumbaku ni pamoja na magonjwa ya moyo, kisukari, figo, kiharusi, upungufu wa nguvu za kiume, vidonda vya tumbo pamoja na magonjwa sugu ya kifua.
Kilimo cha tumbaku pia huathiri sana mazingira; kwa mfano, takwimu zilionyesha kuwa, kati ya mwaka 2010 na 2012, Mkoa wa Tabora, ambao unaongoza kwa kilimo cha tumbaku, ulipoteza misitu yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 10 karibu sawa na sh. bilioni 20, iliyokatwa kwa ajiri ya kukaushia tumbaku.
Kagaruki anasema tumbaku ni tishio kwa maendeleo; hivyo, Chama cha Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku Tanzania.
Ndiyo maana TTCF kinatoa wito kwa serikali kuchukua hatua madhubuti, kuweza kufikia Lengo namba tatu la Malengo ya Maendeleo Endelevu, hasa kwa kuimarisha utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku.
Mkakakti huu, anasema unaweza kutekelezwa kwa kutunga Sheria madhubuti ya kudhibiti matumizi ya tumbaku.
Mfano anasema Serikali pia inashauriwa kuongeza kodi kwenye bidhaa za tumbaku, ili kupunguza uwezo wa vijana kununua bidhaa hizi.
“Zaidi ya hapo, serikali pia izuie uvutaji holela kwenye maeneo ya umma na sehemu za kazi, ili kuwakinga wasiovuta, dhidi ya vifo, maradhi na uzorotaji wa afya vinavyosababiswa na tumbaku,” anashauri Kagaruki.
Anapendekeza mamlaka husika, ziwasaidie wakulima wa tumbaku, waweze kujikita kwenye kilimo cha mazao mbadala, sambamba na kuwatafutia masoko ya mazao hayo.
Udhibiti wa tumbaku, anasema umeoanishwa katika Ajenda ya Maendeleo Endelevu kwa vile unatambulika kama mkakati madhubuti wa kusaidia kufanikisha lengo namba 3.4 la Malengo ya Mendeleo Endelevu la kupunguza theluthi ya vifo vya mapema duniani kote.
Hata hivyo, anasema jukumu hili la kudhibiti tumbaku siyo la serikali pekee bali kila mtu kwa nafasi yake anaweza kufanikisha uthibiti endelevu wa dunia bila tumbaku.
Wavutaji wanaweza kuacha kuvuta, au kutafuta msaada kusaidiwa kufanya hivyo; ili kulinda afya zao na za wale wanaowazunguka.
Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi Wanaokabili Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TJNCDF) kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA). Maoni na ushauri tuma TJNCDF, S.L.P. 13695, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment