Nafasi Ya Matangazo

December 01, 2017

Na Dixon Busagaga 

MWILI uliofukuliwa hivi karibuni kwa kibali cha mahakama kuondoa utata wa taarifa za kupotea kwa Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Scolastica, Humphrey Makundi(16) utazikwa kwa mara ya pili leo (Jumamosi ) . 



Hatua ya kuzikwa kwa mwili huo uliokaa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa zaidi ya siku 14 sasa inatokana na kutoka kwa majibu ya sampuli ya vina saba (DNA) ikionyesha kuwa mwili ni wa Humphrey Makundi.



Kwa mujibu wa baba mzazi wa marehemu Humphrey,Bw Jackson Makundi alisema mazishi yatafanyika katika kijiji cha Mamba kwa Makundi ,Marangu wilaya ya Moshi baada ya kupata kibali cha mahakama cha kuruhusu kuzikwa kwa mwili huo.



Makundi alisema shughuli za mazishi ya mwanae yataoongozwa na maaskofu wasaidizi kutoka Dayosisi ya Dodoma akiwemo mchungaji Samwel Mshana wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) wakisaidiana na Askofu Msaidizi wa (KKKT) dayosisi ya Kaskazini Mchungaji Elingaya Saria.




Novemba  6,mwaka huu taarifa za kutoweka kwa mwanafunzi huyo katika shule aliyokuwa akisoma ya Scolastica iliyopo mji mdogo wa Himo zilianza kuzagaa katika mitandao ya kijamii na baadae Novemba 7 mwaka huu mwili ulikutwa ukiwa umetelekezwa mto Ghona unaokadiliwa kuwa mita 300 kutoka katika shule hiyo.



Mwili huo ambao awali ulifikishwa katika Hosptali ya mkoa wa Kilimanjaro,Mawenzi ulipokelewa na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na baadae kuzikwa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi katika makaburi ya Karanga  kama mwili usiokuwa na ndugu.



Hata hivyo,baada ya kuwepo kwa taarifa ya kuzikwa kwa mwili huo ,familia ya Makundi iliomba kibali cha mahakama kuruhusu  kufukuliwa mwili huo kwa lengo la kujiridhisha ,mtu aliyezikwa kama kweli ni mzee kama taarifa za awali zilivyotolewa au ni ndugu yao. 



Tayari watuhumiwa  watatu kati ya 11 wanao shikiliwa na jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za mauaji ya Mwanafunzi huyo wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi ,Moshi na kusomewa shtaka la mauaji .


Waliofikishwa mahakamani ni pamoja na anayetajwa kuwa mmiliki wa shule ya Scolastica ,Edward Shayo , aliyekuwa mlinzi wa shule hiyo Hamis Chacha na Labani Nabiswa raia wa Kenya anayetajwa kuwa Mwalimu katika shule hiyo.


Mbele ya mahakama ya Hakimu mkazi ,Moshi ,upande wa Jamhuri katika shtaka hilo lililofika mbele ya Hakimu Mkazi ,Julieti Mawore uliwakilishwa na Mwanasheria wa serikali Kassim Nassiri akisaidiana na Wakili wa kujitegemea ,Faygrace Sadallah huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Eliakunda Kipoko anyemtetea Mshatakiwa wa pili katika shtaka hilo Edward Shayo.


Akisoma maelezo ya hati ya mashitaka mbele ya mahakama hiyo ,Nassiri alieleza kuwa mnamo Novemba 6 mwaka huu mshtakiwa wa kwanza ,Hamis Chacha(28),wa pili Edward Shayo (63)  na wa tatu Laban Nabiswa (37) walimuua kwa kukusudia mtu aitwaye Humphrey Makundi.


Kutokana na maelezo hayo Hakimu ,Mawore alieleza kuwa washtakuwa hawaruhusiwi kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikliza shtaka la mauaji huku akiwataka kungojea kufanya hivyo pindi watakapofikishwa mahakama kuu ambapo watapata nafasi ya kuwasilisha mashahidi wao pamoja na kujitetea.


Kuhusu upelelezi wa Shtaka hilo Mwanasheria wa serikali Nassiri aliieleza mahakama kuwa upelelezi haujakamilika huku akiwasilisha ombi la kupangwa tarehe nyingine kwa ajili kutajwa kwa shauri hilo wakati upelelezi ukikamilishwa.


Hakimu Mkazi ,Mawore aliahairisha shtaka hilo na kupanga kutajwa kwa shtaka hilo Desemba 8 mwaka huu  na  kwamba washtakiwa wote watarudishwa Rumande kutokana na  kesi hiyo kutokuwa na dhamana .
Posted by MROKI On Friday, December 01, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo