MBUNGE wa Jimbo la Busega Dk. Raphael Chegeni akizungumza katika mkutano wa hadhara
Na Mwandishi wetu
MBUNGE wa Jimbo la Busega Dk. Raphael Chegeni amewataka vijana na akina mama jimboni Busega kuacha kubweteka na kudai vyuma vimekaza bali waongeze bidii kwa kuchapa kazi kwa nafasi ya kila mtu mmoja mmoja na ndani ya vikundi vyao.
Ushauri huo ameutoa wakati akikabidhi vifaa vya kumwagilia maji mashambani kwa ajili ya kikundi cha vijana wa 'Hapa Kazi Tu' Busega cha Nyanhanga na fedha taaslimu shs Milioni 1, kwa kikundi cha Inuka mama cha Nyashimo.
“Hii ni changamoto kwenu nendeni mkatumie mitaji hii kuwainua kimaisha na muwe mfano kwa vikundi vingine,”alisema Dk Chegeni.
Aidha wakati wa mkutano wa hadhara amechangia sh milioni 10, kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa kwa shule ya Sekondari ya Kata ambayo imepewa jina la Chegeni Secondary School kwa heshima yake na kutambua mchango mkubwa anaoutoa katika kusukuma elimu wilayani humo.
Jumla ya Sekondari 18 zilianzishwa kwa msaada mkubwa kutoka kwake akiwa mbunge na hakuna kiongozi yeyote aliyefanya makubwa upande wa elimu ukilinganisha na yeye.
Wilaya ya Busega inakabiliwa na upungufu wa madarasa kwa wanafunzi 1,209 kwa mwaka ujao wa masomo.
Dk. Chegeni amewataka wananchi na wadau wote kujitoa kutekekeza upatikanaji wa vyumba hivyo.
Aidha amempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa hatua ya serikali yake kuwajali watoto wanyonge wa kitanzania kwa kutoa elimu bure kwa darasa la kwanza hadi kidato cha nne na kuwataka wananchi kuunga mkono jitihada hizo za Rais.
0 comments:
Post a Comment