Anaandika
Dixon Busagaga, Moshi
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa(TAKUKURU)mkoani Kilimanjaro,imemtia mbaroni Daktari wa Hospital ya rufaa
ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi akituhumiwa kudai na kupokea rushwa ya
shilingi 150,000.
Daktari
huyo,Deogratias Godfrey Urio,alikamatwa jana katika mji mdogo wa Himo kwenye
baa maarufu ya Mombasa High Way baada ya
kuwekewa mtego na makachero wa takukuru mkoani Kilimanjaro.
Taarifa
iliyotolewa leo Alhamisi kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Takukuru mkoa wa
Kilimanjaro(RBC),Holle Makungu imesema kuwa kukamatwa kwa daktari huyo
kunatokana na malalamiko ya ndugu wa mgonjwa aliyekuwa akipigwa dana dana
kupatiwa huduma ya upasuaji katika hospital hiyo.
Makungu
ameeleza katika taarifa yake kuwa,mgonjwa huyo alikuwa akihitaji kufanyiwa
upasuaji wa uvimbe katika kizazi chake tangu oktoba mwaka huu baada ya
kufanyiwa vipimo kwenye hospital hiyo na kubainika kuwepo kwa uvimbe.
Lakini licha
ya kubainika kuwepo na uvimbe huo,mgonjwa huyo hakuweza kupata tiba haraka
baada ya kuelezwa na daktari huyo kuwa hawezi kufanyiwa upasuaji huo hadi hapo
atakapotoa fedha hizo.
Makungu
ameeleza kuwa,baada ya taarifa hizo kuwafikia,mtego uliandaliwa na daktari huyo
aliweza kutiwa mbaroni jana Novemba 15 akiwa kwenye baa hiyo ya Mombasa High
Way.
“Tunaendelea
na uchunguzi wa tuhuma hizo na atafikishwa mahakamani mara tu uchunguzi
utakapokamilika,takukuru inatoa rai kwa
madaktari na wauguzi katika hospital ya Mawezi kuzingatia viapo vyao ili
Mawenzi iwe hospital ya kuigwa kwa huduma bora”,amesema makungu.
Mkuu huyo wa
Takukuru mkoa wa Kilimanjaro akahitimisha taarifa yake kwa kuonya kuwa kwa wale
wachache watakaoendelea kutozingatia viapo vyao,watakamatwa na kuchukuliwa
hatua za kisheria na pia kuwataka waajiri wao wachukue hatua kali za kinidhamu
dhidi ya watumishi hao .
0 comments:
Post a Comment