MBUNGE wa Singida Magharibi kwa tiketi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Elibariki Kingu amewafuta machozi akinamama wa jimbo
jirani la Singida Mashariki linaloongozwa na Tundu Lissu wilayani Ikungi, Singida
baada ya kuwanunulia vitanda 52 ili kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto. Anaandika Mroki Mroki/TSN Digital DSM.
Kwa muda mrefu, akinamama hao walikuwa na kilio
cha kukosekana kwa huduma hizo, hasa vitanda vya kujifungulia, hivyo kumlilia
Kingu aliyeamua kubeba jukumu na mbunge mwenzake.
Akizungumza na TSN Digital kwa njia simu, Kingu
alisema ameamua kutoa msaada huo kutokana na maombi aliyoyapata kutoka kwa
akinamama wa eneo la Ikungi na pia kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida juu ya
kuwasaidia katika sekta ya afya kwa kuwapatia vitanda vya kujifungulia.
“Ni kweli ninatarajia siku yoyote nitakwenda
kukabidhi vitanda 86 katika Wilaya ya Ikungi, ambako kuna majimbo ya Singida
Magharibi nilipo mimi na jimbo jirani la Singida Mashariki kwa Tundu Lissu,
kufuatia maombi ya wananchi hasa akina mama ambao huteseka sana kwa kwenda
umbali mrefu kutafuta huduma za afya wakati wa kujifungua,” alisema Kingu.
Kingu alisema kati ya vitanda hivyo 86 vyenye
thamani ya Sh. Milioni 48.9, vitanda 52 atavigawa katika jimbo la Singida
Mashariki na vingine 34 atavigawa katika jimbo lake la Singida Magharibi.
Amesema kati ya vitanda hivyo 52 atakavyovigawa
Singida Mashariki, vitanda 26 ni maalumu kwa ajili ya akinamama kujifungulia na
vitanda vingine 26 kwa ajili ya wodi za kawaida.
Aidha, amesema katika jimbo lake atakabidhi
vitanda 34 vya kujifungulia ambavyo kati ya hivyo, vitanda vinne ni vya kisasa
vinavyotumia umeme.
Wilaya ya Ikungi ina jumla ya Kata 28 ambapo kati
ya hizo, kata 13 zipo katika jimbo la Singida Mashariki ambapo katika sensa ya
watu na makazi ya mwaka 2012 wilaya hiyo ilikuwa na takribani wakazi 272,959.
0 comments:
Post a Comment