Janga la moto lililowakumba wafanyabiashara wa Stendi ya Ngamiani iliyoko Barabara ya 12, Jijini Tanga, limewagusa wadau mbalimbali ambao wamejitolea kuwapa pole na kuwapatia kifuta machozi.
Ajali hiyo iliyotokea usiku wa Agosti 14, 2026, imeleta hasara kubwa kwa wafanyabiashara hao kutokana na bidhaa zao kuteketea kabisa.
Akihitimisha Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, Agosti 24, 2026, katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Jijini humo, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, kipekee alizipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga chini ya uongozi wa Balozi Dk. Batilda Buriani na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Tanga chini ya uongozi wa CPA. Castro John.
Dk. Mwigulu amesema, alipata taarifa ya janga la moto kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Kassim Amar, hivyo anaungana nao katika kuwapa pole wafanyabiashara hao.
"Nikupongeze Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na timu yako, mlienda mkawafuta machozi kidogo wananchi wale waliopatwa na madhila hayo. Niliambiwa umeshawapatia kiasi, basi nitadouble (kuongeza mara mbili ya fedha zilizotolewa) huo mkono uliowashika," amesema Dk. Mwigulu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imekabidhi shilingi milioni 14 kwa wafanyabiashara 12 na familia mbili zilizounguliwa, huku kila mmoja akipata shilingi milioni moja katika mgao huo.
Vilevile, Dk. Mwigulu amewapongeza TRA kwa kuwashika mkono wafanyabiashara hao. "Nawapongeza pia TRA kwa kutoa kifuta machozi, nitoe wito kwa wadau wengine na sekta binafsi kuwaunga mkono TRA," amesema.
Katika salamu za pole, Agosti 18, 2026, Meneja TRA mkoa, CPA John, alisisitiza pamoja na kuwapatia kiasi cha fedha lakini pia watakaa na wafanyabiashara ili kuwasaidia katika kuwapa unafuu wa kodi.









0 comments:
Post a Comment