Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo
Dk. Harison Mwakyembe (wa tatu kulia) akikabidhi bendera ya taifa kwa
wanariadha wa Timu ya Taifa ya Tanzania itakayoshiriki mashindano ya
riadha ya Dunia yatakayofanyika
jijini London wiki hii. Timu hiyo yenye wanariadha nane ambapo watano
kati yao wanashiriki mbio ndefu za Marathon, imeondoka usiku wa leo
kuelekea jijini London. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya
Michezo Dk Omar Singo, Rais wa Chama cha Riadha
nchini Anthony Mtaka, K Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania
ambao ni wadhamini wakuu wa kambi ya maandalizi ya timu hiyo na
aliyemshika mkono Waziri ni Mwanariadha Alphonce Simbu.
************
Timu ya
taifa ya Riadha itakayoshiriki mashindano ya riadha ya Dunia yanayoanza wiki
hii jijini London Uingereza imeagwa na kukabidhiwa rasmi bendera ya Taifa ikiwa
ni ishara ya kuwa wawakilishi maalum wa nchi yetu katika mashindano hayo makubwa.
Timu hiyo
yenye jumla ya wachezaji nane iliagwa jana na Waziri wa Habari, utamaduni Sanaa
na Michezo Harison Mwakyembe katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na maafisa na wadau mbalimbali akiwemo Rais wa chama cha Riadha
Tanzania Anthony Mtaka, Mkurugenzi wa Michezo Dr. Omar Singo na Maharage Chande
- Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania ambao ni wadhamini wakuu wa timu
hiyo.
Akizungumza
wakati wa hafla hiyo Waziri Mwakyembe alisema Wizara yake iko bega kwa bega na
wadau wa michezo hapa nchini katika kuhakikisha kuwa tunapiga hatua katika
sekta hiyo na kuifanya moja ya vyanzo vikubwa vya mapato kwa wanamichezo wetu.
Amesema serikali imejizatiti kikamilikatika kuratibu na kurasimisha michezo
hapa nchini ili wanamichezo watambue kuwa hiyo ni kazi tena ya heshima na yenye
malipo makubwa.
Waziri
mwakyembe pia alionyeshwa kuridhishwa kwakwe na viwango vya wachezaji na
kueleza Imani yake kubwa kuwa wataweza kutuletea ushindi.
“Kwanza kabisa nimetiwa moyo sana na ari ya vijana
waliyonayo na kama mlivyoona na kusikia kwenye vyombo mbalimbali vya habari,
vijana hawa wamepikwa vizuri na wana ari, moyo na uzalendo mkubwa na kilicho
mbele yao ni kitu kimoja tu, kupambana kufa na kupona na kurudi na medali”.
Alisema Waziri na kuongeza “Nilipoangalia viwango vya vijana wa timu yetu ya
taifa nilipata faraja sana. Kwani vijana wote hawa wana viwango vya kimataifa
na ndiyo sababu wakapata tiketi ya kushiriki michuano hii ya dunia. Hili siyo
suala dogo na napenda niwapongeze sana”
Waziri pia
ameipongeza kampuni ya Multichoice Tanzania kwa udhamini wake mkubwa katika
maandalizi ya timu hiyo ambapo kampuni hiyo ilikuwa mdau mkubwa katika
kufanikisha mafunzo katika kambi hiyo.
“Sote tunafahamu kuwa katika mchezo wowote ule duniani,
mazoezi na maandalizi ni kitu cha msingi sana. Kwa kweli, hapa ni lazima nitoe
shukrani za kipekee kwa wenzetu, wadau wa michezo Multichoice Tanzania (DStv)
kwa jitihada kubwa walizozifanya katika kuhakikisha kuwa timu yetu hii
inafanikiwa kufanya mazoezi na maandalizi kwa ajili ya mashindano haya. Ndugu
zetu wa DStv wamejitoa kikamilifu na ndio wadau wakuu walioshiriki katika
kuisaidia kambi ya timu yetu iliyokuwa kule Ilboru Arusha. Huu ni uzalendo wa
hali ya juu kabisa na ninaomba wadau wengine wasisite kushirikiana nasi katika
kuimarisha michezo na Sanaa hapa nchini” Alisema Waziri.
Naye Rais wa chama cha riadha Tanzania Anthony Mtaka,
amesema kuwa mbali na jitihada kubwa zinazofanywa na chama hicho bado zipo
changamoto nyingi ambazo zinahitaji nguvu za pamoja ili kuhakikisha kuwa riadha
inaenda mbele. Amesema kuwa kwa kutambua hilio na kwa kutambua umuhimu wa wadau
mbalimbali, wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu sana na wadhamini pamoja na
majeshi mbalimbali kama vile JKT na JW ambapo wanariadha wengi wanatoka.
Kwa upande
wake Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande amesema
kuwa kampuni yake ina dhamira endelevu
ya kuibua na kuinua vipaji hapa nchini na ndiyo sababu wakaamua kusaidia katika
maandalizi ya timu. “Tumefadhili kwa kiasi kikubwa kambi ya timu iliyokuwa
Ilboru Arusha na pia kuahakikisha kuwa timu inawasili Dar na kujiandaa na
safari ya London” alisema Maharage na kuongeza kuwa “Tumekuwa tukimdhamini
Balozi wetu Alphonce Simbu kwa mwaka mzima sasa. Matokeo ya nguvu zetu
tumeyaona. Ametwaa medali ya dhahabu Mumbai Marathon mapema mwaka huu. Na pia
amevunja rekodi yake London Marathon. Sasa ni miongoni mwa wakimbiaji wa
kutegemewa hapa nchini”.
“Tumeamua
kushiriki kikamilifu kukuza riadha ili kutuwezesha kama taifa kuwa na wigo
mpana wa ushindi kwenye mashindano ya kimataifa. Tuna ndoto ya kutaka kuona na
kuusikia wimbo wetu wa taifa katika mashindano ya Olmpic. Tumeanza, tumeona
matunda, tutaendelea na kuhakikisha ndoto hii inatimia”. Alisisitiza Maharage.
Maharage pia
amesema mbali na udhamini huo, DStv inanawahakikisha watanzania kuona na kuwa
sehemu ya walimwengu wenye bahati ya kuona mashindano makubwa moja kwa moja. “Zamani
kulikuwa ni mambo ya kusimuliwa simuliwa tu… sasa DStv, hatutaki watanzania
wasimuliwe yaliyojiri kwenye duru za michezo ulimwenguni… waone wenyewe. Kwa
jitihada kubwa tumefanikiwa kuwezesha michuano hiii kuonekana katika vifurushi
vyote vya DStv.
Tutazame tuwaone vijana wetu tushangilie ushindi wetu moja kwa
moja bila chenga!” alisema Mkurugenzi huyo na kukumbusha kuwa DStv ilionyesha
mubashara Mumbai Marathon tukamuona Simbu akishinda, DStv ikaonyesha Mubashara London Marathon, tukaona Simbu
akivunja rekodi yake, na kwa mara nyingine tena DStv itaonyesha mubashara
Mashindano haya ya Dunia, ambapo bila shaka kwa timu tuliyonayo, tutashuhudia
tukikwapua medali kedekede na kuliletea taifa letu sifa kubwa.
Akizungumza
mara tu baada ya timu yao kukabidhiwa bendera, mmoja wa wanariadha hao Alphonce
Simbu anayeshiriki mbio ndefu za kilmita 42 amesema kuwa wao wamejiandaa
kikamilifu na wanajua wanabeba dhamana kubwa kwa watanzania wote. Hivyo
watahakikisha kuwa wanapambana na kuleta medali nyumbani.
Amesema
wamejiandaa vizuri na makocha wamefanya kazi kubwa hivyo kilichobaki ni kwa
watanzania wote kuwaombea na pia kuhakikisha wanawashuhudia moja kwa moja
kupitia DStv kuona jinsi wanavyotuwakilisha kwenye mashindano hayo.
Jumla ya wanariada watano watashiriki mbio za
kilomita 42 ambao na Aplphonce Simbu
mwenye rekodi ya 2:09.10-
aliyoiweka hivi karibuni katika London Marathon 2017; Ezekiel Jafari Ng’imba
2:11.55- Hannover Marathon 2017; Stephano Huche Gwandu – 2:14.18 – Tunis Marathon; Sara Ramadhani
Mkera 2:33.08- Dusseldorf Marathon 2017 na Magdalena Crispin Shauri 2:33.28
Hamburg Marathon 2017.
Wakimbiaji watatu waliosalia wanashiriki mbio fupi ambapo
Gabriel Gerald Geay anashiriki mita 5,000; Emanuel Giniki Gisamoda pia
mita 5000 na Failuna Abdi
Matanga wa mita 10,000.
Mashindano hayo yataanza rasmi tarehe 4 Agosti na
yataendelea kwa takriban siku 10.
0 comments:
Post a Comment