Nafasi Ya Matangazo

June 21, 2017


 
 Mkurugenzi  Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bibi. Devota Mdachi akitoa mada katika mkutano nchini Israel alipofanya ziara ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na fursa za biashara kupitia sekta hiyo. Ziara ya siku tatu aliyoifanya nchini humo imeleta ushawishi kwa bodi ya utalii ya Israel kushirikiana na Tanzania katika sekta hii.

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt.Aloyce Nzuki akichangia mada katika mkutano nchini Israel alipofanya ziara ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na fursa za biashara kupitia sekta hiyo. Ziara ya siku tatu aliyoifanya nchini humo imeleta ushawishi kwa bodi ya utalii ya Israel kushirikiana na Tanzania katika sekta hii.
Mkurugenzi  Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bibi. Devota Mdachi akizungumza na waandishi   wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake jijini Dar es Salaam akitoa mrejesho kuhusiana na ziara yao iliyofanyika nchini Israel ikiwa na lengo la kutangaza utalii wa Tanzania iliyofanyika kuanzia Juni 11 hadi 15 mwaka huu.
Mkurugenzi  Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bibi. Devota Mdachi(wapili kushoto) katika picha ya pamoja na  Balozi wa Tanzania nchini Israel Job Massima (wapili kulia) mara baada ya kumaliza mkutano uliowakutanisha wadau wa sekta ya utalii wa nchini Israel kutambua fursa za utalii zilizopo Tanzania. Ziara ya siku tatu aliyoifanya nchini humo imeleta ushawishi kwa bodi ya utalii ya Israel kushirikiana na Tanzania katika sekta hii. Kulia ni Balozi mdogo wa Tanzania nchini Israel Kasbian Chirich na Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt.Aloyce Nzuki. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
***************
Na Mwandishi wetu
BODI ya Utalii Israel imeahidi kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika kutangaza vivutio vilivyopo na kukuza sekta ya utalii nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bibi Devota Mdachi,  aliyeongozana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki, kuitembelea Israeli kwa siku tatu mwezi huu, amesema  ziara yao nchini Israel imeleta mafaikio katika sekta ya utalii  Tanzania.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni  kukutana na wadau wa sekta ya utalii wakiwemo mawakala wa utalii na sekta ya malazi.
“Israel imeonyesha shauku kubwa ya kushirikiana na sisi katika kuutangaza utalii wa Tanzania. Mwaka jana tulipata watalii 22,000 kutoka nchini humo ambapo wameahidi mwaka huu watakuja watalii wengi zaidi.
“Vilevile kupitia vyombo vyao vya habari tumeeleza namna vivutio vyetu vilivyo na mwonekano wa kipekee duniani, tumepokea maombi mengi ya kuja kutembelea fukwe na hifadhi za wanyamapori.”
Alieleza kuwa hifadhi zilizotajwa sana ni Katavi, Mahale, Ngorongoro na Zanzibar: “Tunafahamu Waisraeli wanapenda kuangalia wanyamapori.Nilipokuwa nikiwatajia wanayama tulio nao walionyesha kufurahi hasa nilipowaeleza kuwa faru Fausta (55) mwenye umri mkubwa kuliko wote barani Afrika yupo katika ardhi ya Tanzania walionyesha kuvutiwa zaidi.”
Bw. Nzuki aliuambia mkutano na wadau wa utalii nchini Israel katika Mji waTel Aviv, : “Tanzania kuna fursa nyingi katika uwekezaji,  upande wa hoteli za kitalii.  Ikiwa una kampuni ya kitalii pamoja nyumba ya wageni ya kisasa unajiwekea uhakika wa kupata wageni wengi.
“Ukiwa tayari unaweza kuja na kufuata utaratibu wa kisheria katika mamlaka husika utapewa maelekezo. Tunawakaribisha kuwekeza katika utalii.”
Miongoni mwa wawekezaji wanaofanya shughuli za kitalii nchini , Bwana Alon Hovev anayemiliki kampuni ya utalii ya Sima Safari , ameuambia mkutano huo kuwa sababu zilizomfanya kuwekeza Tanzania ni hali ya hewa na watu wake.
“Watanzania ni wakarimu,  nimevutiwa na mtindo wao wa maisha, vilevile kuna maeneo mengi ya kuvutia ikiwemo pwani safi na mbuga za wanyama,” amesema Bw. Hovev ambaye ameoa raia wa Tanzania.
Utalii ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya mapato nchini, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, ameliambia bunge la bajeti hivi karibuni na kueleza kuwa mwaka 2016 Tanzania ilipokea watalii  milioni 1.2 ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.9 mwaka 2015 walipokuja watalii milioni 1.1.
Mwaka jana sekta ya utalii iliingiza kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 2 ikiwa ni sawa na Sh Trilioni 4, mwaka 2015 iliingiza Dola bilioni 1.9.
Kiwango hicho cha mapato kiliifanya sekta ya utalii kuchangia asilimia 17.5 ya pato la taifa katika bajeti ya mwaka 2016/17 pamoja na kuingiza asilimia 25 ya fedha za kigeni.
Posted by MROKI On Wednesday, June 21, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo