Nafasi Ya Matangazo

May 13, 2017

Siku chache baada ya DStv kutangaza kuwa itarusha moja kwa moja (Mubashara) Michuano ya vijana ya AFCON itakayoanza kesho huko Gabon, habari mpya na njema zinasema sasa DStv itarusha mechi zote za Serengeti boys katika michuano hiyo kwa lugha ya Kiswahili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande, amesema baada ya kampuni yake kuhakikisha kuwa michuano hiyo inashuhudiwa mubashara kupitia DStv, sasa wanataka watanzania wengi zaidi waweze kuifuatilia kwa karibu hususan mechi za timu yetu ya Serengeti Boys, hivyo mechi zote za Serengeti boys zitarushwa mubashara kwa lugha ya Kiswahili.
Amesema watangazaji na wachambuzi mahiri wa mpira wakiwemo Abuubakar Lyongo, Maulid Kitenge, Ephraem Kibonde, Edo Kumwembe na Maestor watashiriki katika zoezi hilo la kuwaletea watanzania burudani hiyo kupitia DStv.
“DStv tunatoa huduma wanayotaka wateja wetu, tunawasikiliza wateja wetu, na kila inapowezekana tunatekeleza matakwa yao” alisema Maharage na kuongeza kuwa baada ya watu kufahamu kuwa DStv itarusha michuano hiyo mubashara, kumekuwa na maombi mengi ya kuangalia uwezekano wa kutangaza michuano hiyo hususan mechi za Serengeti boys kwa Kiswahili.
“Tunaamini kuwa kwa kurusha matangazo hayo kwa Kiswahili, watanzania wa kila kada wataweza kuifuatilia michuano hiyo kwa ukaribu zaidi na hivyo kuongeza burudani ya aina yake katika michuano hiyo” alisema Maharage na kuongeza kuwa pamoja na kutangaza kwa Kiswahili, pia wamehakikisha michuano hiyo inaonekana katika vifurushi vyote kikiwemo cha Bomba cha Sh. 19,975tu ambacho ni miongoni mwa vifurushi nafuu kabisa hapa nchini.
Amewataka watanzania wote kuendelea kuiunga mkono timu yetu kwa kila hali kwani ni muwakilishi wa taifa letu katika michuano hiyo muhimu. “Sisi DStv ni wazalendo wa kweli, ndiyo sababu hatusiti kuunga mkono timu zetu wakati huohuo tukiwahakikishia watanzania fursa ya kushuhudia mashindano mbalimbali mubashara. Enzi za kuangalia micezo iliyonakiliwa imepita, na sisi watanzania tunaenda sambamba na ulimwengu wa kisasa. Kupitia DStv, tunaona vitu mubashara” alisema Maharage.
Serengeti Boys watacheza mechi yao ya kwanza siku ya Jumatatu 15 Mei kabla ya kukabiliana na Angola siku ya Alhamisi 18 Mei na hatimaye Niger siku ya Jumapili 21 Mei.
Kwa mujibu wa majadiliano mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, watanzania wengi wanasubiri kwa shauku michuano hiyo huku ikionekana wazi kuwa wanaimani na Serengeti boys.
Michuano ya AFCON kwa wachezaji wenye umri wa miaka chini ya 17 ya mwaka huu ni ya 12 kwa kuzingatia michuano inayohusisha nchi waandaaji, inayoandaliwa na shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kwa wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 17.  Washindi wane watapata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia la wachezaji wa umri wa chini ya miaka 17 litakalofanyika ncini India mwishoni mwa mwaka huu.
Michuano ya mwaka huu ilipaswa ifanyike nchini Madagascar tarehe 2–16 April 2017 lakini CAF ikaamua kuihamishia Gabon kwa sababu Madagascar haikukidhi vigezo.
Mataifa yaliyofuzu  kushiriki michuano hii mwaka huu ni  wenyeji Gabon, Tanzania, Mali, Angola, Cameroon, Ghana, Guinea, na Niger.
Posted by MROKI On Saturday, May 13, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo