IDADI kubwa ya wahojiwa wa Sauti za Wananchi
(asilimia 78) wameripoti uhaba wa chakula katika maeneo wanayoishi.
Hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini ambako asilimia 84
wameripoti uhaba wa chakula ikilinganishwa na asilimia 64 katika maeneo
ya mijini.
Zaidi
ya nusu ya kaya za Tanzania (yaani asilimia 69) zinahofia kuishiwa
chakula. Aidha asilimia 51 ya kaya zimeripoti kwamba hakukua na chakula
cha kutosha kulisha kaya nzima, au mwanakaya ameshinda na njaa kwa
sababu hakuweza kupata chakula (asilimia 50).
Matokeo haya yalitolewa na Twaweza katika muhtasari uitwao Uchungu wa njaa: Upungufu wa chakula Tanzania. Muhtasari huu umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi,
utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia
njia ya simu.
Takwimu za muhtasari huu zimekusanywa kutoka kwa wahojiwa
1,800 wa Tanzania bara (Zanzibar haikuhusishwa kwenye matokeo haya) kati
ya tarehe 14 na 26 mwezi wa tisa, 2016 na kutoka kwa wahojiwa 1,610
kati ya tarehe 9 na 15 mwezi wa pili 2017.
Kwa
mujibu wa wananchi wengi, uhakika wa kupata chakula umepungua kati ya
mwezi Septemba 2016 na Februai 2017: Mwezi wa pili 2017, asilimia 65 ya
wananchi walikuwa na hofu ya kaya zao kukosa chakula cha kutosha ikilinganishwa
na asilimia 45 waliosema hivyo mwezi Septemba 2016. Mwezi Februari
2017, asilimia 51 ya wananchi waliripoti kwamba kuna wakati hawakua na chakula cha kutosha kwa ajili ya kaya zao
katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Kabla ya hapo, mnamo mwezi
Septemba 2016, asilimia 43 ya wananchi iliripoti kwamba hali kama hiyo
iliwatokea katika kipindi cha miezi kumi na miwili iliyopita.
Mwezi
Februari 2017, asilimia 35 ya wananchi waliripoti kuwa na mwanakaya
angalau mmoja alieshinda na njaa siku nzima kwa sababu ya kukosa chakula katika
kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Hili ni ongezeko kutoka asilimia 21
walioripoti kwamba hali hiyo iliwatokea katika kipindi cha miezi sita
tangu Aprili mpaka Septemba 2016.
Takwimu
za Benki Kuu ya Tanzania zinaonesha kwamba bei ya mahindi (halisi,
jumla) imeongezeka mara mbili (baada ya kuirekebisha na kiwango cha
mfumuko wa bei wa wakati huo) katika kipindi cha miaka miwili iliyopita
kutoka shilingi 400 kwa kilo mwanzoni mwa 2015 mpaka shilingi 852 mwezi
wa kumi na mbili, 2016. Wahojiwa wa Sauti za Wananchi wameripoti kwamba
kwa wastani kilo moja ya mahindi inawagharimu shilingi 1,253. (Bei
zilizoripotiwa kwenye masoko ya ndani).
Upungufu
na uhaba wa chakula unaoendelea ni kielelezo cha hali ngumu ya maisha
iliyopo na umasikini wa kipato. Jumla ya watu nane kati ya kumi
(asilimia 80) wameripoti kwamba kaya zao hazina kipato cha kutosha
kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza anasema:
“Wananchi wamekumbwa vikali na upungufu wa chakula. Tumepokea mwitikio
wa serikali katika suala hili na tunaunga mkono jitihada za kuzuia maafa
makubwa. Hata hivyo, takwimu zinaonesha kwamba wananchi bado wanaishi
kwenye hali ngumu na wamejaa hofu ya kukosa chakula. Jitihada za
kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania yeyote anayelala njaa zishike nafasi
ya kwanza katika vipaumbele vyetu vya kitaifa.”
0 comments:
Post a Comment