Nafasi Ya Matangazo

January 22, 2017

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya umma (PIC) Mhe. Albert Obama (kushoto) akisalimiana na Afisa mtendaji mkuu wa Dawasco Mhandisi Cyprian Luhemeja (kulia) mara baada ya kamati hiyo kuwasili katika Ofisi ya Dawasco Makao Makuu jijini Dar es Salaam, ili kujionea shughuli mbalimbali zinazoendeshwa na shirika hilo.
***************
KAMATI ya kudumu ya bunge ya uwekezaji wa mitaji ya umma (PIC), imesema kuwa Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) lina uwezo wa kumaliza tatizo la Maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kutokana na mitambo ya uzalishaji Maji ya Ruvu juu na Ruvu chini kuwa ya Kisasa na yenye uwezo mkubwa wa kuhudumia mikoa hiyo.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Albert Obama, ambaye pia ni mbunge (CCM) wa jimbo la Buhingwe, mara baada ya kamati hiyo kuhitimisha ziara yake ya siku moja ya kutembelea mitambo ya uzalishaji Maji wa Ruvu Juu na Ruvu Chini iliyopo Mkoani Pwani.
   
Alisema kuwa, kamati hiyo imeshuhudia uwekezaji mkubwa kwenye miradi hiyo, hivyo kuridhishwa na kazi inayofanywa na shirika na kwamba wakazi wa Dar es Salaam na Pwani, wanaweza kuhudumiwa endapo uwekezaji huo utakamilika kwa asilimia 100.
   
"Tumeona kazi kubwa, nzuri inayofanywa na Dawasco na Dawasa, ikiwamo miradi mikubwa ya Ruvu Juu na Ruvu Chini ambapo mradi mkubwa wa juu utakapokamilika mwaka huu utasaidia kuondoa kero ya Maji kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na Pwani itakuwa historia." alisema.

Aidha alisema kamati hiyo imeishauri DAWASCO kubuni mbinu bora ya kuzuia upotevu wa Maji, ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo wake wa usambazaji Maji ambao umekuwa na mivujo mingi hivyo kupelekea Maji mengi kupotea.
Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO, Mhandisi Cyprian Luhemeja, alisema kuwa ziara ya kamati ya Bunge imekuja wakati mwafaka ambapo Shirika hilo linapambana kumaliza tatizo la upotevu wa Maji katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam na Mkoa wa Pwani.

“Tumeanza kufanya jitihada za makusudi za kupambana na upotevu wa Maji ikiwa ni pamoja na kubadilisha dira zote za zamani za Maji pamoja na miundombinu yote ambayo ni chakavu" alisema.

Nao wajumbe wengine wa kamati hiyo,Wamefurahishwa na namna ambavyo DAWASCO wanavyofanya kazi ya uzalishaji na utibuji Maji kwa ufanisi na utaalamu wa hali ya juu.
Posted by MROKI On Sunday, January 22, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo