Nafasi Ya Matangazo

November 15, 2016

 Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto (WLAC), Theodosia Muhulo (kulia) akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi zao zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, leo kuhusu kuiomba Serikali kubadilisha sheria ya Mirathi ya Kimila inayomkandamiza Mwanamke wakati inapotokea mume kufariki. Kushoto ni Mkurugenzi wa Umoja wa Wajane Tanzania (TAWIA) Rose Sarwatt.

Aidha Muhulo, alisema kuwa kumekuwa kukitokea matukio kadhaa ya kunyanyaswa wajane pindi anapofariki mume, ambapo alitoa takwimu kuwa hadi sasa mkoa unaoongoza kwa matukio hayo ni Mkoa wa Mbeya Wilaya ya Kyela.
Mkutano ukiendelea 
Mkutano ukiendelea
Mkurugenzi wa Umoja wa Wajane Tanzania (TAWIA) Rose Sarwatt (kushoto) akizungumzia kuhusu Wajane waliofanyiwa matukio ya kunyanyaswa na ndugu wa mume baada ya mume kufariki. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
Mjane Elizabeth Stefano mkazi ya mkoani Mbeya, akitoa ushuhuda wa mambo aliyofanyika na shemeji yake mdogo wa marehemu mumewe.
Mjane Salome Charles, kutoka Mbeya akitoa ushuhuda wa mambo aliyofanyika na wanandugu wa mume.
******************
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UTEKELEZAJI WA MRADI WA UPATIKANAJI WA HAKI KWA WANAWAKE KUPITIA MKATABA WA CEDAW NA ONGEZEKO LA MASHAURI YA MIRATHI YALIYORIPOTIWA WLAC NA KATIKA VITUO VYA WASAIDIZI WA KISHERIA VINAVYORATIBIWA NA WLAC.

Ndugu wanahabari,
Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) ni Shirika lisilo la kiserikali linalotoa huduma ya msaada wa sheria kwa wanawake na watoto, kujenga uelewa wa jamii juu ya sheria na haki za binadamu hususani haki za wanawake na watoto ili kuondokana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuishawishi serikali ili kutunga sera na sheria zenye mtazamo wa kijinsia. Kwa takribani miaka 27 sasa, WLAC imekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma hii ya msaada wa sheria ambapo maelfu ya wanawake wenye matatizo ya kisheria wameweza kufaidika.

Ndugu wanahabari,
Kuanzia Mwezi Oktoba, 2015, WLAC imekuwa ikitekeleza mradi wa upatikanaji wa haki kwa wanawake kupitia mkataba wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW). 

Mradi huu ulianza baada ya WLAC kupata tuzo mnamo kutoka katika kamati ya Umoja wa Mataifa ya Mkataba wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW) kutokana na taarifa iliyowasilishwa na WLAC katika kamati hiyo kuhusu kesi mkakati ya kupinga Sheria ya Mirathi ya Kimila inayowanyima wajane fursa ya kurithi. 

Kupitia mradi huo, WLAC kwa kushirikiana na wasaidizi wa kisheria pamoja na wadau wengine wa haki za binadamu imeweza kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuelimisha jamii kuhusu sheria zinazohusu masuala ya wanawake na watoto (hususani watoto wa kike) kama vile Sheria za Mirathi, na uwepo wa Mikataba mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa kama vile Mkataba wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) ambayo nchi yetu imeridhia na namna ya kutumia mikataba hiyo kudai haki za wanawake na watoto (hususan watoto wa kike)

Ndugu wanahabari,
Katika kutekeleza mradi huo, WLAC iliweza kufanya midahalo mbalimbali katika mkoa wa Dar es Salaam na Shinyanga ambapo imefikia watu zaidi ya 200 (mia mbili).

Kufanyika kwa midahalo hii katika mkoa wa Shinyanga ni kutokana na ukweli kwamba, huu ndio mkoa ambao wanaishi wajane wawili (ambao wapo hapa leo) walioathiriwa moja kwa moja na Sheria ya Mirathi ya Kimila kwa kunyimwa usimamizi wa mirathi pamoja na kunyang’anywa mali zilizoachwa na marehemu waume zao. 

Wajane hawa ndio waliosaidiwa na WLAC kufungua kesi mkakati ya kupinga Sheria ya Mirathi ya Kimila ambayo ni ya kibaguzi. 
Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam mnamo mwaka 2005 na kutolewa uamuzi mwaka 2006.

Katika uamuzi huo, Mahakama ilikubaliana na ukweli kuwa baadhi ya vifungu vya sheria hiyo ni vya kibaguzi lakini ikasema kwamba “haiwezekani kufanya mabadiliko ya kimila kwa tamko la kisheria”. 

Mahakama pia ilidai kwamba, kubadili Sheria ya Kimila kutakuwa ni chanzo cha matatizo mengi yasiyofikiriwa yatakayoibuka kutoka katika mila zote za kibaguzi zilizopo katika makabila zaidi ya 120. 

Mahakama iliamua kuwa, njia bora ya kurekebisha hali hiyo ni kupendekeza kwamba halmashauri za Wilaya zirekebishe sheria za kimila.

Ndugu wanahabari,
Uamuzi huu wa Mahakama umeendelea kugharimu maisha ya wajane na watoto wa kike kwani bado upatikanaji wa haki za mirathi kupitia Sheria ya Mirathi ya Kimila umekuwa mgumu japo mahakama zimekuwa zikijitahidi kutumia busara zaidi ya sheria. 

Hata hivyo, katika kutekeleza mradi huu wa upatikanaji wa haki kupitia mkataba wa CEDAW, WLAC imeendelea kukutana na ukiukwaji wa haki za wajane kutokana na jamii kuendelea kushikilia mila na desturi ambazo zinamnyima mjane na mtoto wa kike fursa ya kurithi. 

Vile vile, kumekuwa pia na ongezeko la mashauri ya mirathi yaliyoripotiwa WLAC na katika vitengo vya wasaidizi wa sheria vinavyoratibiwa na WLAC. Kwa mfano kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, WLAC (Kupitia huduma ya msaada wa sheria kwa njia ya simu na kliniki zake za Dar es Salaam, Kasulu, Kibondo na Muleba) imeweza kupokea mashauri mapya ya Mirathi 243 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 8.6 % ukilinganisha na mashauri 222 yaliyopokelewa mwaka 2015. 

Vile vile wateja 578 wa mwendelezo wenye mashauri ya mirathi walihudumiwa katika kipindi hicho cha Januari hadi Oktoba 2016. 

Hivyo,kufanya idadi ya mashauri yote ya mirathi yaliyopokelewa katika kituo kufikia 821. Kwa upande wa wasaidizi wa kisheria kutoka mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida, Tabora,Shinyanga, Mwanza, Kigoma, Iringa, Mbeya, Rukwa, Lindi na Mtwara, idadi ya mashauri 811 ya mirathi yaliweza kupokelewa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Oktoba, 2016. 

Wasaidizi wa kisheria kutoka mkoa wa Mbeya –Wilaya ya Kyela wameonekana kuongoza kwa kupokea mashauri 153 ya mirathi. 

Hii inadhihirisha wazi kwamba tatizo la mirathi bado ni kubwa katika jamii na hivyo jitihada madhubuti zinahitajika ili kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa haki kwa wajane na watoto ikiwemo kuwepo kwa Sheria ya Mirathi inayoheshimu haki za wanawake na kuthamini usawa.

Hivyo basi, Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) kwa kushirikiana na Wasaidizi wake wa Kisheria, Chama cha Wajane Tanzania(TAWIA), Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wajane na Watoto (CWCA) pamoja na wajane walioathiriwa na Sheria ya Mirathi ya Kimila, kinatoa wito kama ifuatavyo:

1. Serikali kulipa kipaumbele suala la marekebisho ya Sheria ya Mirathi ya Kimila kwani sheria iliyopo ni ya kibaguzi na kandamizi kwa wanawake na watoto wa kike hivyo kuchangia kurudisha nyuma jitihada za mwanamke kujikwamua kiuchumi. 

Hata hivyo, Sheria hii inakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (Kama ilivyofanyiwa mabadiliko ya mara kwa mara) na Mikataba mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa kuhusu haki za wanawake na watoto ambayo serikali yetu imeridhia. 

2. Serikali kutekeleza mkataba wa CEDAW kwa kuufanya kuwa sehemu ya sheria za nchi.

3. Serikali kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW) kupitia Taarifa Na. 48/2013 ambayo ilihusisha malalamiko yaliyowasilishwa na wajane wawili ambao wameathiriwa na Sheria ya Mirathi ya Kimila. 

4. Serikali kutoa elimu kwa jamii ili kuondokana na mila potofu dhidi ya wanawake na watoto na kuwatendea haki badala ya kuwanyanyasa kwa namna mbalimbali.

Tamko hili limetolewa na Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) kwa kushirikiana na wasaidizi wa kisheria wa mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Kigoma, Iringa, Mbeya, Rukwa, Lindi na Mtwara, Chama cha Wajane Tanzania(TAWIA) na Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wajane na Watoto (CWCA).


ASANTENI KWA KUTUSIKILIZA

IMESAINIWA
THEODOSIA MUHULO
MKURUGENZI MTENDAJI (WLAC)
Posted by MROKI On Tuesday, November 15, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo