MAMLAKA ya Mapato Tanzania
(TRA) imeanzisha vituo vinavyohama katika jitihada za kukabiliana na msongamano
wa wananchi wanao hakiki na kuboresha taarifa za Namba ya Utambulisho wa
Mlipakodi (TIN) katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Pamoja na kutumia vituo
vinavyohama, TRA pia inaendelea kuongeza idadi ya vituo na vifaa vya utendaji ili
kuhakikisha wananchi ambao hawajahakiki na kuboresha taarifa zao wanafanya
hivyo kabla ya tarehe ya mwisho ya uhakiki ambayo ni 30 Novemba 2016
Kituo kimojawapo
kilichoongezwa ni cha Kimara Mwisho ambapo pamoja na kufanya shughuli za
uhakiki kituo cha Ofisi ya Kimara ambacho kimefunguliwa rasmi hivi karibuni
kitatoa huduma zingine za kodi ikiwa ni pamoja na usajili wa Kodi ya Ongezeko
la Thamani (VAT), malipo ya kodi za magari, malipo ya kodi za mapato ikiwemo
Kodi za Kampuni, kodi za watu binafsi, kodi za mishahara, kodi za uendelezaji
ufundi stadi na ushuru wa stempu.
TRA inawasihi wananchi
wanaohakiki taarifa zao kuwa makini kwani TRA imebaini kuibuka wananchi
wasiowaaminifu ‘vishoka’ ambao wanatumia mwanya wa msongamano wa wanachi katika
vituo vya uhakiki kuwalaghai na kusababisha usumbufu usio wa lazima.
Katika kuhakikisha kuwa
wafanyabiashara wanatendewa haki wanapopata huduma TRA hasa wakati wa
makadirio, TRA inawaasa kutambua kwamba wanayo haki ya msingi kukata rufaa
katika ngazi mbalimbali kwa kuanzia na Meneja wa Mkoa husika au kwa Kamishna
kutegemea na aina ya kodi na hatimaye kwa Kamishna Mkuu endapo wataona haki
haijatendeka.
Katika hatua nyingine TRA imeendelea na jukumu la ukusanyaji wa mapato
ambapo imekusanya jumla ya shilingi Trilioni
1.150 kipindi cha mwezi
Oktoba 2016 na kufanya makusanyo yote ambayo TRA imekusanya kwa mwaka wa fedha 2016/17
kufikia shilingi Trilioni 4.752 hadi
sasa.
Pamoja na mafanikio hayo ya
makusanyo ya kodi TRA pia imepata mafanikio katika rufaa za kesi
zinazowasilishwa kwa uamuzi zaidi katika baraza ra Rufani za kodi katika
kipindi cha mwezi Oktoba baada ya kushinda kesi tisa zenye thamani ya kodi ya
shilingi billioni 16.941.
Jumla ya kesi 27 zinazohusu
masuala mbalimbali ya kodi ziliwasilishwa katika Baraza la Rufani za Kodi kwa
uamuzi ambapo kesi kumi zimeamuliwa na kati ya hizo ni kesi moja tu ambayo
mlipakodi alishinda. Kesi nyingine bado zinaendelea kusikilizwa.
Ushindi huu wa kesi
unadhihirisha jinsi TRA inavyofanya makadirio ya kodi kwa umakini haki na
weledi bila kumuonea mtu yeyote.
‘Pamoja
Tunajenga Taifa Letu’
Richard
M. Kayombo
MKURUGENZI
HUDUMA NA ELIMU KWA MLIPAKODI
0 comments:
Post a Comment