Nafasi Ya Matangazo

February 20, 2026






Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefanya Ziara yake leo kwa kutembelea miradi ya umeme na imeipongeza Serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, uongozi na wafanyakazi wa TANESCO kwa kazi na hali ya uzalishaji wa umeme, ambapo sasa nchi ina uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 4,400.

Kwenye Ziara hiyo iliyofanyika Februari 20,2026  ambapo ilitembelea Kituo cha Kusafirisha Umeme kwenda Zanzibar cha Ras Kilomoni na Kituo cha kuzalisha Umeme kwa Gesi Asilia cha Kinyerezi I na II.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amesema kumekuwa na maendeleo makubwa katika eneo la uzalishaji wa umeme, na sasa TANESCO inaendelea na jitihada za kujenga njia za kusafirisha umeme, ikiwemo ya kutoka bwawa la Julius Nyerere hadi Chalinze, kisha Kinyerezi hadi Mkuranga, eneo lenye viwanda vingi vya uzalishaji.

“Tunaipongeza sana TANESCO kwa utekelezaji wa miradi ya umeme. Ile hali ya kukatika kwa umeme imepungua, na sasa hakuna mgao. Kamati inashauri kuwa nguvu kubwa sasa itumike katika kuhakikisha umeme unamfikia mlaji wa mwisho, hususani katika maeneo ya viwanda na migodi,” alifafanua Mhe. Subira.

Naye Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mhe. Innocent Luoga, amesema wamepokea maagizo ya Kamati kuhusu maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 nchi iweze kuzalisha jumla ya megawati 8,000.

“Hivi sasa mahitaji ya umeme yameendelea kuongezeka, hasa katika shughuli za uzalishaji. Serikali kupitia TANESCO, inahakikisha umeme unawafikia wananchi, na lengo ni kuwaunganishia umeme takribani wananchi milioni 1.7 kwa mwaka.”

Kwenye ziara hii Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeahidi kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuweza kufikia malengo na mipango inayotekelezwa hapo mbeleni.






Posted by MROKI On Friday, February 20, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo