Nafasi Ya Matangazo

February 19, 2026



Na OWM - KAM Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu amewataka Mawakala binafsi wa Ajira kuzingatia mwongozo wa uratibu wa ajira za nje ya nchi ili watanazania wengi wanufaike na fursa za ajira zinazozalishwa.

Waziri Sangu ameyasema hayo Dar es Salaam jana (19 Februari 2026) wakati alipofanya mkutano na Mawakala binafsi 148 wa ajira za ndani na nje  uliolenga kutoa mwelekeo wa Serikali kuhusu uzingatiaji wa uratibu wa kisheria na kimfumo.

“Zamani kulikuwa uholela na ndio maana mmeniletea changamoto ya vishoka, Serikali haitambui uwepo wa hao vishoka .Hivyo  tumeanzisha mifumo ya kisheria na ya kitaasisi inayosimamia ajira za ndani na nje ya nchi” alisisitiza Waziri Sangu.

Aliongeza kusema Serikali ya Awamu ya Sita inatambua jukumu la Mawakala binafsi kuwa ni nguzo muhimu ya kuwaunganisha watafutaji kazi na waajiri ndani na nje ya nchi pia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini na kusaidia nchi  kujenga uchumi shindani, jumuishi na endelevu.

Akizungumza kwa niaba ya Mawakala binafsi , Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala Binasfi wa Ajira Tanzania (TRAA) Mohammed alisema chama hicho ni mshirika wa serikali katika kupunguza ukosefu wa ajira na kuongeza mapato ya taifa na kuongeza hadhi ya Mtanzania anaefanya kazi nje .

Mwenyekiti huyo alisisitiza jukumu la TRAA ni kuona ushirikiano wa karibu kati ya serikali na wadau wa maendeleo ya sekta za ajira za kimataifa inaendelezwa ili kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa letu.

Kwa upande wake Kamishna wa Kazi Bi. Suzan Mkangwa amesema uwepo wa mwongozo huo ni moja ya hatua za serikali katika kuimarisha huduma za ajira nchini na kwamba ushiriki wa mawakala 148 na kwenye kikao hicho cha Waziri no kutimiza malengo ya Serikali katika kuimairisha mahusiano na kuongeza uwelewa juu ya wajibu wao kisheria na kulinda maslah ya watafuta kazi na maslahi ya taifa kiujumla.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Jane Sorogo amesema kufanyika kwa kikao hicho ni mwendelezo wa Idara ya Huduma za Ajira katika kutekeleza dhamira ya pamoja ya Serikali na wadau  kuimarisha mifumo ya ajira iliyo salama, halali na yenye kulinda utu na maslahi ya Mtanzania. 

Kupitia ushirikiano huu Bi. Sorogo alisema Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kujenga mazingira ya uwazi, uwajibikaji, katika kufikia tija na ufanisi katika kuratibu huduma za ajira ndani na nje ya nchi ambapo lengo ni kutimiza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongeza fursa za ajira kwa watanzania wengi zaidi nje ya nchi.

Itakumbukwa hivi karibuni Waziri Sangu alipokuwa akizungumza na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi, Waajiri na Shirikisho jijini Dodoma alitaja mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwa kwa kipindi cha Januari 2026 hadi sasa takribani watanzania 2002 wamepata fursa za kwenda kuajili nje ya nchi na jumla ya madereva magari 1,150 wamemaliza usaili wa nafasi za kazi nchini Qatar pia kuna madereva pikipiki 500 wanatarajiwa kwenda nchini Falme za Kiarabu (UAE) chini ya uratibu wa mawakala binafsi wa ajira na Serikali.
Posted by MROKI On Thursday, February 19, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo