CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa majonzi na simanzi kubwa taarifa za kifo cha Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania, Samuel John Sitta, kilichotokea usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alikokuwa akitibiwa.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, imesema, Samuel John Sitta, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za utumishi katika Chama na Serikali. Alikuwa Katibu wa CCM na Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Mkuu wa kituo cha uwekezaji, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Mjumbe wa Kamati Kuu, Mbunge, Waziri na Spika.
Taarifa hiyo imesema, Sitta alikuwa ni Kiongozi mchapakazi, mwadilifu na aliyejitambulisha kwa utendaji wenye kufuata falsafa yake ya “kasi na viwango”. Ametoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Chama na Serikali.
Kufuatia kifo hicho, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amemtumia salamu za rambi rambi Spika wa Bunge la Job Ndugai, familia na Wananchi wa Jimbo la Urambo. "Tunaungana nao katika msiba huu ambao pia ni msiba wetu, Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, Ameni", Amesema Kinana akikaririwa na taarifa hiyo.
0 comments:
Post a Comment