Nafasi Ya Matangazo

September 23, 2016



Meneja wa Shirika la Umeme mkoani Kigoma, Masigija Lugata (katikati) akimweleza jambo Waziri wa Nishati na Madidi, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) wakati wa ziara yake Wilayani Kankonko mkoani Kigoma. Wapili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala.
Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya State Grid Company anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini (REA II) wilayani Kakonko mkoani Kigoma kuhakikisha anarekebisha kasoro zote zilizo bainika katika mradi huo kabla ya kuukabidhi hapo tarehe 30 mwezi huu.

Wito huo umetolewa jana wilayani humo wakati alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Awamu ya Pili Mkoani Kigoma ambapo alibaini changamoto mbalimbali ikiwemo ya nguzo za umeme kusimikwa vibaya bila kuzingatia utaalamu hasa ikizingatiwa kuwa maeneo hayo hua na upepo mkali unaoweza kusababisha nguzo hizo kuanguka.

Katika ziara hiyo, Profesa Muhongo alipatiwa taarifa na Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Col. Hosea Ndagala ambaye alimueleza kutoridhishwa na namna mradi huo unavyotekelezwa ikiwemo uduni katika usimikaji wa nguzo za umeme.

Alisema baadhi ya nguzo hizo zimeanza kuinama kutokana na upepo na kutokana na nguzo hizo kusimikwa bila ubora hali inayoweza kusababisha madhara kwa Wananchi wa eneo hilo endapo nguzo hizo zitadondoka.

Kufuatia taarifa hiyo na ukaguzi alioufanya kwenye eneo la mradi, Waziri Muhongo aliagiza hadi kufikia mwisho wa Mwezi huu Mradi huo uwe umekabidhiwa kwa Meneja wa TANESCO Kigoma na kwamba kabla ya kupokelewa Mkuu wa Wilaya naye athibitishe kuridhishwa utekelezaji wake ikiwemo kurekebisha kasoro zilizobainika ili wananchi wanufaike na mradi ulio katika ubora unaotakiwa.

Profesa Muhongo alisema endapo Mkandarasi atashindwa kutatua changamoto hizo na kasoro zilizo jitokeza katika mradi huo hatoruhusiwa kushiriki katika utekelezaji wa Mradi wa REA III ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya  Awamu hii ya pili kukamilika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya State Grid, Wilboad Mutabuzi alisema mradi huo wa Kakonko anaoutekeleza umekamilika kwa asilimia 98 na huku akiahidi kuhakikisha anashughulikia kasoro zilizobainika ili akamilishe mradi kwa wakati na wenye ubora unaokubalika.

Mutabuzi alisema gharama za mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) kwa mkoa wa Kigoma ni shilingi bilioni 23 na kwamba katika Wilaya ya Kakonko vijiji saba vimefaidika na mradi huo.

Alisema  changamoto kubwa iliyojitokeza ni muitikio mdogo wa Wananchi kuunganishiwa huduma ya nishati ya umeme kutokana na sababu mbalimbali.

Alisema kutokana na muitikio wa wananchi kuwa mdogo imesababisha kushindwa kufikia lengo ambapo kwa Mkoa mzima wa Kigoma lengo lilikuwa ni kuwaunganishia huduma ya umeme wateja wapatao 11,000  lakini hadi sasa ni wateja 7,000 tu ndio waliopatiwa huduma husika.
Posted by MROKI On Friday, September 23, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo