Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia
Wakandarasi, Wahandisi na wadau mbalimbali wa sekta ya Ujenzi kabla ya kufungua
rasmi Mkutano wa Siku mbili wa
Mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini CRB uliofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitembelea maoneshio ya zana za ujenzi baada ya
kufungua mkutano wa siku mbili wa Mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi
jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipewa maelezo
kuhusu katapila linalotumika katika kazi mbalimbali za ujenzi mara baada ya
kufungua mkutano wa siku mbili wa Mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi
jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia vifaa
vya ujenzi katika moja ya mabanda mara baada ya kufungua mkutano wa siku mbili
wa Mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi jijini Dar es Salaam. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
*******************
RAIS wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakandarasi kote nchini
kufanya kazi kwa kutanguliza maslai ya taifa, badala ya kutaka kupata faida
kubwa kupita kiasi kutoka kwenye zabuni za miradi ya ujenzi wanayopata kutoka
serikalini.
Dkt. Magufuli
amesema hayo leo tarehe 26 Mei, 2016 alipokuwa akifungua mkutano wa mashauriano
wa bodi ya usajili wa wakandarasi kwa mwaka 2016 unaofanyika kwa siku mbili
katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es salaam.
Rais Magufuli
amesema serikali yake ipo tayari kuwapa kipaumbele wakandarasi wa Tanzania pale
inapotangaza zabuni za miradi ya ujenzi, lakini amewataka kujirekebisha kwa
kupanga viwango vinavyostahili vya gharama za ujenzi wa miradi hiyo ambavyo
serikali itaridhika.
"Nawatolea
mfano, idara ya mahakama imetangaza kujenga mahakama za mwanzo na za wilaya,
kwenye bajeti wana shilingi bilioni 24, makadirio ya kitaalamu yanaonesha kila
jengo lisizidi shilingi milioni 200, wakandarasi wazalendo walipoomba katika
nyaraka zao wametaka jengo moja lijengwwe kwa shilingi bilioni 1 na milioni 400,
sasa nakuuliza Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu wakandarasi, hata kama una upendeleo,
upendeleo huo utapasua moyo.
"Hata kama
utakuwa na upendeleo kiasi gani kwa wazalendo utashindwa, sasa mimi niwaombe
ndugu zangu wakandarasi, pamoja na nia nzuri ya serikali kuwasaidia wakandarasi
wazalendo ni lazima na ninyi muwe na nia nzuri ya kuisadia nchi"
Amesema Rais Magufuli
Pamoja na hilo,
Rais Magufuli ametaka wakandarasi hao kuacha kutoa rushwa kwa watendaji wa
serikali pale wanapoomba zabuni za ujenzi na badala yake amewataka kutoa
taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) ili watendaji hao
wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
"Mimi
niwaombe wakandarasi, msikubali kutoa rushwa, na muwafichue watendaji wanaoomba
rushwa, atakapokuomba wewe rushwa hujui amewaomba wangapi, na utakapotoa rushwa
huna hakika kama ile tenda utaipata, wengine wameishia kutoa rushwa hapa,
rushwa hapa, rushwa hapa mpaka anafilisika, kazi huipati na rushwa umeitoa"
Amesisitiza Dkt. Magufuli.
Aidha, Rais
Magufuli ametoa wito kwa wakandarasi hao kujipanga ipasavyo ili waweze kupata
zabuni katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi itakayofanywa hapa nchini
ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya
Tanga hapa Tanzania, Ujenzi wa Reli ya Kati na Ujenzi wa Viwanda.
"Sina uhakika
kwamba mmejipangaje wakandarasi wa Tanzania katika kuhakikisha hiyo kazi
mnaipata ya kujenga bomba kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.
"Nitasikitika
sana kilometa zote 1,410 pasiwepo mkandarasi hata mmoja wa kutoka Tanzania,
wenzetu wanajipanga, na ninavyoona wakandarasi wa Tanzania wameendelea sana,
lakini nashindwa kuelewa kuna tatizo gani linatufanya kutojua changamoto
zinazotukabili, tumejipanga kujenga reli ya kati (Standard Gauge) kwenye bajeti ya mwaka huu tunaanza na
kilometa 100, lakini kuna fedha nyingine zitatolewa na serikali ya China,
tutajenga zaidi ya kilometa 1,200 (Standard Gauge, Central Corridor) itakayounganisha Mwanza, Kigoma, Burundi
na Rwanda. Wakandarasi wa Tanzania mmejipangaje? ameuliza
Rais Magufuli.
Mkutano huo pia
umehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
TAKUKURU Kamishna Valentino Mlowola ambaye amesema Taasisi hiyo ipo tayari
kukabiliana na rushwa iliyopo katika sekta ya ujenzi ambayo ni miongoni mwa
sekta zenye rushwa kubwa na ametaka wakandarasi watoe ushirikiano kukomesha
tatizo hilo.
0 comments:
Post a Comment