Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa
wa Shinyanga Bi. Anne Kilango Malecela
na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Abdul Rashid Dachi, kufuatia mkoa huo kutoa
taarifa zisizo sahihi kuwa hauna watumishi hewa.
Rais Magufuli
ametangaza kutengua uteuzi wa Viongozi hao wa Mkoa wa Shinyanga leo tarehe 11
Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam, mara baada ya kupokea Taarifa ya Mwaka
2014/2015 ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na kupokea
hundi kifani ya shilingi Bilioni 6 kutoka Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania zilizotokana na kubana matumizi.
Dkt. Magufuli
ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa kuwa Mkoa wa Shinyanga hauna watumishi
hewa, aliamua kutuma timu ya ukaguzi iliyokwenda kufanya uchunguzi ambapo hadi
kufikia jana tarehe 10 Aprili, 2016 imebaini kuwepo watumishi hewa 45 huku
zoezi likiwa linaendelea katika wilaya mbili za Ushetu na Shinyanga Vijijini.
"Na wale wote
wa Shinyanga ambao walisemekana ni zero, hakuna mtumishi hewa, walikuwa tayari
wameshalipwa shilingi milioni 339.9, nimejiuliza sana, na nikajiuliza sana na
kwa kweli nimejiuliza sana na kwa masikitiko makubwa, kwa nini Mkuu wa Mkoa
alisema hakuna mtumishi hewa?" Amesisitiza Rais
Magufuli
Rais Magufuli amesema
baada ya kutengua uteuzi wake, Anne Kilango Malecela atapangiwa kazi nyingine.
Pamoja na hatua
hiyo, Dkt. Magufuli ametaka wakuu wa mikoa yote wawafichue watumishi hewa wote
ili waondolewe mara moja, na ameagiza timu iliyofanya uchunguzi Mkoani
Shinyanga itumike kufanya uchunguzi katika mikoa mingine kwa lengo la kukomesha
upotevu mkubwa wa fedha za umma.
Katikati ya Mwezi
Machi, 2016 Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa yote nchini kusimamia zoezi
la kuwaondoa watumishi hewa wote katika orodha ya malipo ya mshahara, ambapo
mpaka tarehe 31 Machi, 2016 Jumla watumishi hewa 5,507 walibanika.
Kati ya shilingi
Bilioni 583 ambazo serikali imekuwa ikitumia kila mwezi kwa ajili kulipa
mishahara, kati ya shilingi Bilioni 53 na 54 zimekuwa zikipotea kutokana na
kulipa mishahara ya watumishi hewa.
Kabla ya kutangaza
kutengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Rais
Magufuli ameipongeza ofisi ya Bunge kwa kubana matumizi na kufanikiwa kuokoa
shilingi Bilioni 6, ambazo zitatumika kutengeneza madawati ya wanafunzi wa
shule na amezitaka ofisi na taasisi nyingine za serikali kuiga mfano huo.
Ameagiza fedha
hizo zipelekwe Idara ya Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili vyombo
hivyo vifanye kazi ya kutengeneza madawati yanayotarajiwa kuwa zaidi ya 120,000
ambayo yatasambazwa katika shule ili kukabiliana na tatizo la wanafunzi
wanaokaa chini kwa kukosa madawati.
Hundi Kifani ya
fedha hizo imekabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Akson, ambaye amesema Ofisi ya Bunge
imetekeleza wito wa serikali wa kubana matumizi ambapo kiasi hicho cha shilingi
Bilioni 6 kimepatikana kwa kipindi kifupi cha takribani nusu mwaka.
Katibu wa Bunge
Dkt. Thomas Kashilila ametaja maeneo ambayo Bunge limebana matumizi kuwa ni
Safari za nje ya nchi, Mafunzo nje ya nchi, Machapisho na ununuzi wa majarida,
Shajala, Chakula na Viburudisho, Mtandao, Malazi hotelini, Matibabu ya wabunge
na familia zao nje ya nchi, Umeme, Maji, Simu na Uendeshaji wa Mitambo.
0 comments:
Post a Comment