Nafasi Ya Matangazo

March 31, 2016

 Vijana wakikusanya pumba za mpunga kwa ajili ya kuziuza kwenye kiwanda cha TBL cha Mwanza
Meneja wa kiwanda cha TBL cha Mwanza akionyesha mashine inayotumia pumba za mchele.
********
MIAKA michache iliyopita pumba za  mpunga hazikuwa na matumizi makubwa badala yake zilikuwa  takataka za kuchoma moto baada ya kupembuliwa na kutolewa zao la mchele.

Hivi sasa katika kanda ya ziwa pumba zimegeuka kuwa lulu kutokana na kupata soko ambapo zinauzwa na kuwapatia fedha wafanyabiashara wanaomiliki mashine za kusaga nafaka na wakulima wadogo wadogo wanaojishughulisha na kilimo cha mchele.

Thamani ya pumba ambazo awali zilionekana takataka kuwa lulu inatokana na uwekezaji unaozingatia utunzaji wa mazingira uliofanywa na kampuni ya TBL Group kwa kuleta mashine zinazotumia pumba hizo kuzalisha nishati katika kiwanda cha kutengeneza bia kilichopo mjini Mwanza.

Uwekezaji huu pia umeleta manufaa kwa jamii ya wananchi wa kanda ya ziwa ambao hivi sasa wanakiuzia kiwanda pumba za mpunga .

“Hizi pumba za mpunga unazoona tunakusanya hapa sio kwa ajili ya kuzitupa ama kuwagawia wafugaji waziweke kwenye mabanda ya kuku kama ilivyokuwa siku za nyuma bali tunaziuza kwa wafanyabiashara ambao nao wanaziuza kwenye kiwanda cha kutengeneza bia cha Mwanza kwa ajili ya kutumika kuzalisha nishati ya umeme,” alisema Bi.Tausi Jumanne mkulima na mfanyakazi katika mashine ya kusaga mchele inayojulikana kama Umoja iliyopo mjini Kahama.

Akiongea kwa niaba ya wanawake wenzake wanaofanya biashara hiyo  alisema kuwa hivi sasa kilimo cha mchele ni mali kwa maana baada ya kusaga mpunga bado wakulima wananufaika kwa kuuza pumba na kujiongezea kipato. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA.
John Ngosha mkulima na mkazi wa Katoro wilayani Geita anasema kuwa zamani matumizi ya pumba za mpunga hayakuwa makubwa ila kwa sasa yameongezeka na kilimo cha mchele kinalipa kwani baada ya kupata mchele bado wanauza pumba na kujipatia fedha za ziada zinazowasaidia kupunguza ukali wa maisha.

“Tunashukuru uwekezaji uliofanywa na kampuni ya bia ya TBL Group kwa kujenga kiwanda mkoani Mwanza ambao kwa kiasi kikubwa unatunufaisha  wakazi wa kanda ya ziwa ambapo tumeanza nasi kupata mapato kutokana na uwekezaji huu kwa kukiuzia malighafi”.Alisema Ngosha kwa niaba ya wenzake.

Aliongeza kuwa uwepo wa kiwanda hicho umesaidia kuongezeka kwa ajira na mzungumko wa fedha. “Kiwanda kimesaidia kwa mambo mengi zaidi ya sisi wakulima wadogo kuuza pumba na mashudu maana kuna wafanyabiashara wengi wanakiuzia malighafi mkoani hapa”.Alisema.

Meneja wa kiwanda hicho Richmond Raymond Anasema kuwa utaratibu uliowekwa kununua pumba hizo kwa ajili ya kuzalisha nishati ya kuendeshea mashine ni mzuri na wakulima wanaonekana kuufurahia.

 Alisema mafanikio  haya ya kufanya uzalishaji usiochafua mazingira wakati huohuo kunufaisha wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya kiwanda yanayopakana na kiwanda ni moja ya  mikakati  ya uwekezaji ya kampuni ya SABMiller yenye mwelekeo wa Maendeleo endelevu na kanuni za pamoja.

Moja ya malengo hayo aliyataja kuwa ni Dunia yenye nuru njema,lengo  hili limelenga kuharakisha ukuaji wa kampuni na maendeleo ya kijamii katika mfululizo wake wa maadili.

Pia kampuni imelenga kutekeleza malengo ya kujenga  dunia imara na dunia iliyo safi ambayo yamelenga kupata raslimali ya pamoja ya maji ya kutosha ambayo inatumika kwa kiasi kikubwa katika biashara ya kampuni.

Katika kutekelea lengo hili kampuni kwa muda mrefu imekuwa mstari wa mbele  kulinda na kutunza vyanzo vya maji na kuhakikisha maji yanayopatikana yananufaisha jamii ya wananchi inayowazunguka.

Lengo lingine pia ni kujenga dunia yenye nguvu kazi lengo kubwa likiwa ni kusaidia matumizi bora na endelevu ya ardhi kwa mazao ya bia vinywaji vyenye kilevi na visivyo na kilevi. Katika kutekeleza lengo hili ,wakulima wa zao la  shayiri zaidi ya 30,000 wamekuwa wakinufaika kwa kuuza mazao yao kwa kampuni ikiwa ni moja ya mkakati wake wa kuwawezesha watanzania kwa kununua malighafi yanayotumika katika uzalishaji kutoka kwa  kampuni za hapa nchini na wananchi wa Tanzania.


Malengo haya ambayo baadhi yake yanashabihiana na malengo  endelevu ya Umoja wa Mataifa yanadhihirisha kuwa kampuni ya TBL Group ni kampuni iliyodhamiria kufanya uwekezaji wenye kuleta tija na mabadiliko kwa jamii ya  watanzania.
Posted by MROKI On Thursday, March 31, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo