Nafasi Ya Matangazo

February 23, 2026

 
Uwepo wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) umetajwa kuwa chachu ya kupungua kwa uingizaji na usambazaji wa bidhaa bandia katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususan bandarini na mipakani. Hatua hiyo imeelezwa kuimarisha ulinzi wa watumiaji na kuweka mazingira rafiki ya ushindani wa haki sokoni.

Serikali imeipongeza FCC kwa juhudi zake za kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa bidhaa, ikisisitiza kuwa kazi hiyo ina mchango mkubwa katika kulinda afya za wananchi na kukuza uchumi wenye misingi ya ushindani sawa.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika ufunguzi wa kikao kazi kati ya FCC na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Mpogolo amesema mafanikio hayo yanaonyesha wazi umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za serikali na wadau mbalimbali, hususan wanahabari, katika vita dhidi ya bidhaa bandia. Ameeleza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuibua na kufichua vitendo vinavyohatarisha afya na uchumi wa wananchi.

Hata hivyo, ameihimiza FCC kuongeza kasi ya operesheni zake, hasa katika maeneo yenye shughuli kubwa za kibiashara kama Soko Kuu la Kariakoo na maeneo mengine ya jiji, ambako bado kuna changamoto ya uwepo wa bidhaa zisizo halali sokoni.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa FCC, Amina Ngasongwa, amepongeza mchango wa vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusu madhara ya bidhaa bandia na kusisitiza umuhimu wa watumiaji kuwa makini kabla ya kufanya maamuzi ya ununuzi.

Kikao kazi hicho kililenga kuimarisha ushirikiano kati ya FCC na wahariri wa vyombo vya habari, kwa lengo la kuongeza uelewa wa umma na kuendeleza mapambano dhidi ya bidhaa bandia nchini. 
Source: Madelemonews Blog. 

Posted by MROKI On Monday, February 23, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo