Nafasi Ya Matangazo

February 15, 2016

Ukifika mkoani Mbeya eneo la Iyunga kilipo kiwanda cha kutengeneza bia cha TBL na kufanikiwa kuingia kiwandani hapo utajisikia uko eneo tofauti kutokana na mandhari utakayokutana nayo  kuanzia majengo ya kiwanda ,mwonekano wa wafanyakazi ambao wengi wao ni vijana, mazingira ya ndani ya kiwanda na yaliyokizunguka bila kusahau mitambo ya kisasa ya  uzalishaji iliyopo kiwandani hapo.

Kiwanda cha TBL tawi la Mbeya kilichopo chini ya kampuni ya TBL Group  ni miongoni mwa viwanda bora vya kutengeneza bia barani Afrika kinachoongozwa na msomi wa kitanzania mwenye fani ya Uhandisi katika fani ya umeme wa Viwandani Mhandisi  Waziri Jemedari.

Katika mahojiano yaliyofanyika hivi karibuni Mhandisi Jemedari ameeleza kuwa anaipenda kazi yake na anajisikia furaha kuongoza kiwanda kikubwa cha TBL Mbeya  ambacho ni miongoni mwa viwanda bora vya kutengeneza bia katika bara la Afrika kikiwa kimeajiri hazina ya vijana wasomi wa kitanzania ambao wanamudu vizuri kazi zao.BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI
“Kiwanda hiki ni miongoni mwa viwanda bora vya kutengeneza bia barani Afrika na kina rekodi ya kushikilia nafasi ya kwanza kwa kuwa kiwanda bora, hivyo unapokuwa kiongozi wa kiwanda kama hiki inatakiwa kuhakikisha viwango vyake katika sekta zote vinabaki kuwa juu ,kazi ambayo naifanya kwa kushirikiana na timu ya wafanyakazi wenzangu wote kuhakikisha tunaendelea kuweka rekodi nzuri”.Alisema

Aliongeza kusema kuwa Kutokana na historia hii ya ubora barani Afrika, kiwanda kimekuwa kikiendelea kufanya vizuri na kinavutia wageni kutoka  sehemu mbalimbali ambao wamekuwa wakikitembelea mara kwa mara  kwa ajili ya kujionea mafanikio na kujifunza.

Siri ya kiwanda hiki kuwa  kiwanda bora alisema kuwa kilipoanzishwa kilifungwa vifaa na mitambo ya kisasa ya uzalishaji vilevile kilianza kutumia kanuni bora za uendeshaji viwanda kwa njia ya kisasa za kampuni ya SABMiller ambayo ndiyo inamiliki kampuni mama ya  TBL Group.

Alisema kanuni hizi zinazojulikana kitaalamu kama The Manufacturing Way  zinaelekeza mfumo wa uzalishaji bora wenye viwango na wenye kuleta tija,na kugusa maeneo yote ya uendeshaji  viwanda kwa ufanisi wenye kuleta matokeo bora na zikifuatwa na kutekelezwa ipasavyo lazima matokeo yake yawe mazuri na mafanikio yapatikane.

“TBL Group  hivi sasa inatumia kanuni hizi katika viwanda vyake vyote na matokeo yake yanaonekana kuanzia kwenye uchangiaji wa pato la taifa kupitia kodi,kuwa mwajiri bora,kusaidia masuala mbalimbali ya kijamii,kuwezesha wakulima wanaouzia kampuni malighafi za kutengenezea vinywaji,kuzingatia kanuni za usalama kazini,kupunguza tatizo la ajira nchini na mengineyo mengi”.Alisema.

Pia alisema mfumo huu unaenda sambamba na kampuni kuajiri vijana wa kitanzania ambao wanapatiwa fursa ya kuonyesha vipaji vyao na wanaendelezwa kwa kupatiwa mafunzo mbalimbali ambapo wanafanya kazi kwa ufanisi na kuleta matokea mazuri “TBL Group ni tanuru la kuendeleza vipaji na ina mfumo wa  kuajiri wafanyakazi waliobobea kwenye fani mbalimbali ambao wanaendana na viwango vya kampuni na mchango wao na ufanisi wao katika kazi kuongeza mafanikio.

Kuhusiana na historia yake Jemedari  anasema kuwa ni Mzaliwa wa mkoani Mara ambaye alipata  elimu ya msingi na sekondari na baadaye kujiunga na.Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisomea shahada ya kwanza ya Uhandisi wa umeme.
 Mbali na shahada ya Uhandisi  akiwa mwajiriwa wa TBL amehudhuria kozi mbalimbali nje ya nchi ambazo zimezidi kumpatia maarifa katika fani yake na kumfanya awe miongoni mwa wahandisi nguli wanaoaminika nchini katika fani ya umeme wa viwanda hususani vinavyozalisha vinywaji.

Baadhi ya kozi ambazo zimemnoa zaidi kitaalamu alisema kuwa alizipata katika  nchi za Afrika ya Kusini na  nchini Ujerumani bila kusahau mafunzo ya ndani anayoendelea kuyapata kiwandani hapo kwa sasa
Kuhusiana na historia yake ya kazi anasema kuwa alijiunga na TBL mwaka  mwaka 1999 kama mhandisi wa umeme na  baada ya kutumikia kiwanda hicho kwa kipindi kirefu akiwa ameshikilia nafasi mbalimbali za uongozi kwenye idara yake. Alijiunga na kampuni ya Coca Cola Kwanza kwa ajili ya kupata ujuzi zaidi ambako alifanya kazi kazi kwa muda mfupi na kurejea tena TBL ambako anaendelea kufanya kazi hadi leo akiwa Meneja wa Kiwanda.

Mafanikio aliyoyapata akiwa mfanyakazi wa TBL amesema kuwa ni mengi ikiwemo kuhudumia familia yake vizuri pia amejifunza mambo mengi yanayomsaidia kuendesha maisha na yatakayomsaidia kimaisha hata baada ya kustaafu kazi.

Kuhusu changamoto anazokabiliana nazo katika kazi yake alisema ni za kawaida na anaamini kuwa hakuna kazi isiyokuwa na changamoto kinachotakiwa na kuangalia namna ya kukabiliana nazo.

Mbali na kazi yake ya utawala na uhandisi umeme baada ya saa za kazi anapendelea kusoma vitabu mbalimbali ikiwemo kujishughulisha na ufugaji “Napenda sana shughuli za ufugaji na mara nitakapostaafu  kazi nitakuwa mfugaji vilevile kujishughulisha na utoaji wa ushauri wa kitaalamu kuhusiana na fani yangu ya umeme.


Jemedari anatoa wito kwa vijana wa kitanzania kutokimbia masomo ya hesabu na sayansi wanapokuwa mashuleni bali wajitahidi kukomaa nayo kwa kuwa  katika dunia hii ya sayansi na teknolojia bila wataalamu wa kutosha katika nyanja mbalimbali itakuwa vigumu kwa taifa kupiga hatua ya maendeleo na pindi watakapoajiriwa au kujiajiri wafanye kazi kwa bidii.
Posted by MROKI On Monday, February 15, 2016 1 comment

1 comment:

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo