Nafasi Ya Matangazo

February 15, 2016

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue
****
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa mabalozi watatu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.

Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa makamishna wanne wa Jeshi la Polisi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, imewataja mabalozi walioteuliwa kuwa ni Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro, Mheshimiwa Mathias Meinrad Chikawe na Dkt. Ramadhan Dau.
Vituo vya uwakilishi kwa mabalozi hawa vitajulikana baada ya taratibu husika za kidiplomasia kukamilika.

Kwa upande wa Makamishna wa Polisi, Balozi Sefue amewataja walioteuliwa kuwa ni:

    1. Naibu Kamishna wa Polisi Simon Nyakoro Sirro ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi, na ameteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam. Kamishna Sirro anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Mstaafu Suleiman Kova.

   2. Naibu Kamishna wa Polisi Albert Nyamuhanga ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Fedha, Utawala na Lojistiki. Kamishna Nyamuhanga anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi Clodwing Mathew Mtweve aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza.

   3. Naibu Kamishna wa Polisi Robert Boaz Mikomangwa ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Intelijensia. Kamishna Mikomangwa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Valentino Mlowola aliyeteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

   4.  Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Nsato Marijani Mssanzya ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Mafunzo na Operesheni. Kamishna Mssanzya anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi Paul Moses Chagonja aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi.

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Modestus Francis Kipilimba kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). 

Kabla ya Uteuzi huu Dkt. Kipilimba alikuwa Mkurugenzi wa Menejimenti ya Udhibiti (Director of Risk Management) katika Benki Kuu ya Tanzania. Dkt. Kipilimba anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Dikson Maimu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Teuzi zote zinaanzia leo tarehe 15 Februari, 2016
Posted by MROKI On Monday, February 15, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo