Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Januari, 2016 amewasili
Mkoani Arusha ambapo keshokutwa tarehe 23 Januari, 2016 atatunuku kamisheni kwa
maafisa wanafunzi wa kundi la 57/15 katika chuo cha mafunzo ya kijeshi (TMA)
Monduli mkoani hapa.
Rais Magufuli
amewasili Mjini Arusha akitokea Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(KIA) alikotua kwa ndege akitokea jijini Dar es salaam na kupokelewa na mamia
ya wananchi.
Akiwa uwanjani
hapo Rais Magufuli amewashukuru wananchi kwa mapokezi makubwa aliyoyapata na
amewaeleza kuwa uchaguzi umekwisha, kilichobaki ni kazi tu.
"Nawashukuru
sana ndugu wananchi kwa mapokezi haya makubwa, naomba kuwahakikishia kuwa
uchaguzi umekwisha na sasa kilichobaki ni kuchapa kazi tu"
Alisema Rais Magufuli.
Akiwa njiani
kutoka uwanja wa ndege wa KIA, Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa
njiapanda ya KIA, Kikatiti, Usa River, Tengeru na Mount Meru Mjini Arusha
ambapo huko kote pamoja na kusisitiza kuwa uchaguzi umekwisha na kilichobaki ni
kuchapa kazi, amewahakikishia kuwa hatawaangusha.
Dkt. Magufuli
ametoa wito kwa watanzania kumuombea ili aendelee kuwashughulikia wote wanaofanya
ubadhilifu wa fedha za umma kupitia kampeni yake ya kutumbua majipu.
"Nataka
niwahakikishieni kuwa nitaendelea kutumbua majipu yote mpaka yaishe, na naomba
mniombee ili kazi hii ya kutumbua majipu ifanyike kwa mafanikio"
Alisisitiza Mheshimiwa Magufuli.
Aidha Rais
Magufuli amesema tayari serikali imeanza kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia
elimu ya Msingi na Sekondari baada ya kufuta ada na akaonya kuwa watumishi wa
umma hususani wakuu wa shule watakaothubutu kufanya ubadhilifu wa fedha hizo
watashughulikiwa.
Amesema yote
aliyoyaahidi kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na watanzania kwa ujumla ikiwemo
ujenzi wa barabara za Arusha, kulipa fidia za wananchi na kufuta ada ya shule
za msingi na sekondari yanatekelezwa.
Rais Magufuli
amesisitiza kuwa serikali yake haitawabagua watanzania kwa dini zao wala
makabila yao na wala haitawabagua kwa milengo ya vyama vyao na kanda zao na
kuwataka watanzania wote kuiweka mbele
Tanzania na kushirikiana kuiendeleza.
Gerson
Msigwa.
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha.
21 Januari,
2016
0 comments:
Post a Comment