Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Magufuli akijadiliana jambo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini General
Davis Mwamunyange wakati akielekea kupewa maelezo ya zoezi zima la Onesha Uwezo
Medan.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Magufuli akisalimiana na baadhi ya Maafisa wa jeshi katika tukio hilo la
Ufungaji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Magufuli akielekea kwenye uwanja wa maonesho akiwa pamoja na Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi Nchini General Davis Mwamunyange.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa ngazi za juu wa Jeshi
mara baada ya kufunga zoezi la Onesha Uwezo Medani Monduli Mkoani Arusha.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katikati
akishuhudia matukio ya zoezi la Onesha Uwezo Medani Monduli Mkoani Arusha.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipewa
maelezo ya zana mojawapo ya Kivita katika Zoezi la Onesha Uwezo Medani Mkoani
Arusha. BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI
******************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefunga "Zoezi la Onesha Uwezo
Medani" lililoandaliwa na kutekelezwa na Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu
ambalo ni sehemu ya Jeshi la wananchi Tanzania katika eneo la Lang'arurusu nje
kidogo ya Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli Mkoani Arusha.
Akizungumza na Askari na
Maafisa wa Jeshi la wananchi Tanzania kabla ya kufunga zoezi hilo, Rais
Magufuli amesema katika awamu yake ya tano ya uongozi amedhamiria kulitumia
Jeshi la wananchi Tanzania katika kujenga uchumi, ikiwemo kuanzisha viwanda na
kampuni za ujenzi ili kuharakisha maendeleo.
Ametoa mfano wa kiwanda cha
Nyumbu ambacho kipo chini ya jeshi la wananchi Tanzania na kueleza kuwa wakati
umefika wa kukiimarisha na kukiendeleza kiwanda hicho, ili kiweze kufanya
uzalishaji mkubwa kwa manufaa ya nchi ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa.
"Zipo nchi nyingi ambazo
majeshi yao yanatumika katika uchumi na yanafanya kazi nzuri ya kupigiwa mfano,
wakati umefika na sisi kufanya hivyo. Hata hizi sare za jeshi na viatu, hatuna
sababu ya kuvinunua kutoka nje ya nchi, tunaweza kutengeneza sisi wenyewe"
Alisisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli amelipongeza
Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuandaa "Zoezi Onesha Uwezo
Medani" ambalo limethibitisha uwezo, weledi na utayari lilionao katika
jukumu lake la kiulinzi.
Ameahidi kuwa ataendeleza
juhudi zilizofanywa na viongozi wenzake waliotangulia za kuliimarisha kwa
vitendea kazi na maslai ya wanajeshi ili liweze kutekeleza wajibu wake bila
vikwazo.
Pamoja na kuwapongeza Askari
na maafisa wa Jeshi la wananchi Tanzania walioshiriki katika zoezi hilo, Rais
Magufuli ameagiza Askari Mgambo na Askari wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT)
walioshiriki zoezi hilo kuajiriwa na jeshi la wananchi Tanzania.
Akitoa maelezo ya awali kabla
ya hotuba ya Rais Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt.
Hussein Ali Mwinyi, amesema Wizara yake itaongeza na kusimamia juhudi za
kuliboresha jeshi hilo kwa zana, vifaa na maslai kwa wanajeshi ili kuwajengea
uwezo na morali ya kutekeleza majukumu yao ya kuilinda nchi, pamoja na kutoa
msaada stahiki kwa nchi zenye kuhitaji ulinzi wa amani popote duniani.
Kwa upande wake Mkuu wa
majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange amemhakikishia Rais
Magufuli kuwa Jeshi la wananchi Tanzania lipo imara na litaendelea kutekeleza
majukumu yake kwa weledi, nidhamu ya hali ya juu na uzalendo mkubwa.
Kabla ya kuwahutubia maafisa
wa jeshi la wananchi, Askari na wananchi waliohudhuria ufungaji wa "Zoezi
Onesha Uwezo Medani", Rais Magufuli ameoneshwa zana mbalimbali za kivita
ikiwa ni pamoja na kushuhudia upigaji wa mizinga ya masafa mafupi, masafa ya
kati na masafa marefu.
0 comments:
Post a Comment