Kwa
mujibu wa Sheria ya Sikukuu za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap
35) pamoja na Sheria zingine zinazompa mamlaka Rais kutangaza siku
yoyote kuwa sikukuu au mapumziko, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameamua kuwa
maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na Jamhuri zitakazofanyika tarehe 9
Desemba, 2015, yatumike kwa kufanya kazi.
Kwamba
maadhimisho ya Uhuru ya mwaka huu (2015) yatatumika kama kichocheo cha
kujenga tabia ya kufanya kazi (Uhuru na Kazi) katika Taifa letu.
Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa
kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini, sokoni,
viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi
kwa vitendo.
Aidha,
kwa kuwa Sherehe za Uhuru na Jamhuri huendana na Maandalizi mbalimbali
ambayo yanatumia fedha, kwa kuzingatia kuwa siku hiyo itaadhimishwa kwa
kufanya kazi, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo
sasa zitumike kwa shughuli zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na
kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia dawa za hospitali,
vitanda vya hospitali n.k. kadri kamati za maandalizi zitakavyoamua.
Ieleweke
kuwa sherehe za Uhuru na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha
kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu. Hivyo, sherehe hizi zitaendelea
kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia mwaka 2016.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
0 comments:
Post a Comment