Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Shaban Ally Lila akitoa ufafanuzi
kuhusu Kichwa cha Habari ya Mahakamani kilichoandikwa bila kuzingatia Weledi na
moja ya Gazeti la Kila siku wakati wa
mafunzo ya siku mbili ya Waandishi wa
Habari za Mahakama yaliyofanyika jijini Dar es salaam. Picha/Aron Msigwa –MAELEZO.
*******
MAHAKAMA ya Tanzania imesema kuwa itendelea kufanya kazi na vyombo vya
Habari nchini katika kuuhabarisha umma kuhusu utekelezaji wa jukumu la Kikatiba
ililonalo la kutafsiri sheria mbalimbali na kuzitolea maamuzi ili kuwawezesha
wananchi kujua na kupata Haki zao kwa wakati.
Akifunga Mafunzo ya siku 2 ya waandishi wa Habari za Mahakama jana
jijini Dar es salaam Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Shaban Ally
Lila aliwataka waandishi hao kutimiza wajibu wao wa kuueleza umma taarifa
sahihi za mashauri mbalimbali yanayotokea mahakamani kwa kuzingatia sheria.
Alisema vyombo vya habari na mahakama vinahitajiana, vinafanya kazi
pamoja kwa manufaa ya umma huku akieleza kuwa mikutano ya mara kwa mara kati ya
wanahabari na mahakama kunaongeza kuaminiana na kujenga mahusiano mazuri. HABARI ZAIDI BOFYA HAPA
Alifafanua kuwa kazi ya Mahakama kikatiba ni kutafsiri sheria mbalimbali
na kuzitolea maamuzi kwa mujibu wa sheria kulingana na mashauri
yananayowasilishwa Mahakamani na kuongeza kuwa hakuna Jaji wa Mahakama ya
Tanzania anayeamua kesi bila nje ya utaratibu wa sheria zilizopo.
Alisema wao kama majaji hutumia sheria zilizopo katika kutoa maamuzi
hata kama haziwapendezi wahusika na kuongeza kuwa jambo wanalolifanya ni kutoa
maoni na mapendekezo kwa mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.
" Sisi kama Majaji hutumia sheria zilizopo kutoa maamuzi,hatutungi
sheria jukumu letu kikatiba ni kutafsiri sheria mbalimbali na kuzitolea maamuzi
pia tunatumia fursa ya maamuzi tunayoyatoa kuelimisha jamii kuhusu sheria
iliyotumika kutoa haki katika kesi husika" Alisema.
Aliwataka waandishi wa Habari za Mahakama kujipa muda wa kutosha pindi
wanapofika Mahakamani kufuatilia mashauri yanayoendeshwa ili waweze kuwa na
taarifa za kutosha pindi shauri linapofunguliwa na kutolewa hukumu ili
kuwawezesha wananchi kupata taarifa za kutosha za mwenendo wa Mashauri.
Aliongeza kuwa Mahakama ya Tanzania imedhamiria kufanya kazi na
waandishi wa habari nchini kwa kuzingatia kwamba wakati majaji wanapotoa hukumu
mahakamani kunakuwa na idadi ndogo ya wananchi wanaoshuhudia kuliko ile iliyo
nje ila vyombo vya habari kutokana na umuhimu wake huwapasha habari mamilioni
ya watanzania walio nje ya Mahakama.
Alisema Mahakama itaendelea kujenga mahusiano mazuri na Vyombo vya
Habari hususan waandishi wa Habari za Mahakama kwa kutenga maeneo ndani ya
Mahakama yatakayotumiwa na waandishi hao kuwawezesha kufanya kazi zao bila
vikwazo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Pia alieleza kuwa Mahakama, itaendelea kutoa taarifa za ufafanuzi wa
hukumu mbalimbali zitakazotolewa kwa vyombo vya habari pia Nakala za taarifa za
Hukumu kwa waandishi wa habari ili kuwawezesha wananchi kujua ukweli wa yale
yanayojili mahakamani kuondoa upotoshaji unaotokea.
Aidha alisema kuwa Mahakama itaendelea kushirikiana na Baraza la
Habari Tanzania (MCT) katika kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa
habari za Mahakama ili waweze kuandika habari zenye ukweli na uhakika.
Mhe. Shaban Lila alisema kuwa Mahakama iko tayari kupokea maoni
yanayohusu utendaji kazi wake ili iweze kuyafanyia kazi kwa manufaa ya vyombo
vya habari na wananchi.
Awali akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo kabla ya kumkaribisha
Jaji Kiongozi kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Mahakama ya
Tanzania Bi. Wanyenda Kuta aliwaambia washiriki wa mafunzo hayo kuwa Mahakama
inaendelea kutekeleza nguzo 3 ambazo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na
Upatikanaji wa Haki kwa Wakati, Kuongeza Imani wanachi kwa Mahakama pia
kuboresha miundombinu ya Mahakama nchini.
Alisema kuwa wandishi wa Habari za mahakama waliohudhuria mafunzo hayo
yaliyoandalia na Mahakama ya Tanzania na Baraza la Habari Tanzania (MCT)
wamejifunza masuala mbalimbali ambayo yamewajengea ufahamu waandishi wa Habari
za Mahakama kuhusu lugha za kimahakama, uandishi bora wa habari za Mahakama,
Uhuru wa Mahakama pamoja na kujua Haki za Washitakiwa na Watuhumiwa
wanapofikishwa mahakamani.
Kwa upande wake Meneja wa Maadili wa Baraza la Habari Tanzania (MCT)
Allan Lawa akizungumza na wanahabari hao aliwataka waandike habari za
Mahakama kwa usahihi na umakini mkubwa kufuatia Mafunzo waliyoyapata.
Bw. Lawa aliishukuru Mahakama mafunzo hayo na hatua ya uongozi wa
mahakama kuyakubali mapendekezo yaliyotolewa na Waandishi wa Habari za
Mahakama ikiwemo kutenga eneo ndani ya mahakama litakalotumiwa na waandishi wa
Habari za Mahakama, utoaji wa Nakala za kesi na ufafanuzi wake mara hukumu
zinapotolewa, Mahakama kukubali kushawishi uanzishaji wa madawati ya Habari za Mahakama
kwenye vyombo vya Habari pamoja na mahakama kukubali kuendesha mafunzo ya mara
kwa mara kwa waandishi wa Habari za Mahakama na wahariri wao.
0 comments:
Post a Comment