Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw.
Ephraim Kwesigabo akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu Mfumuko wa Bei wa
Taifa kwa mwezi Machi 2015 ambao umefikia asilimia 4.3 leo jijini Dar es
salaam. Kushoto niKaimu Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi hiyo Bi.
Ruth Minja.
*************
Na Veronica Kazimoto,
Takwimu
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Machi 2015 umeongezeka kidogo
hadi kufikia asilimia 4.3 ikilinganishwa na asilimia 4.2 za mwezi Februari kutokana
na kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa taarifa ya mfumuko
huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa ongezeko hilo linatokana na
badiliko la bei ya bidhaa na huduma kati ya mwezi Machi na Februari 2015.
Amesema bei ya vinywaji
baridi na bidhaa za vyakula ikiwemo Mchele, Ungawa Muhogo, nyama, Samaki,
Maharage, Choroko na Sukari kwa mwezi Machi imeongezeka kidogo ikilinganishwa na
ile iliyokuwepo mwezi Februari.
Amesema Mfumuko wa Bei unaopimwa
kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.7 mwezi Machi ikilinganishwa na
ongezeko la asilimia 1.6 za mwezi Februari huku Fahirisi za bei kwa mwezi Machi
zikiongezeka hadi 155.88 kutoka 154.83 za mwezi Februari, 2015 kutokana na ongezeko
la bei ya mchele, Samaki, matunda aina ya machungwa, maharage, mboga mboga na sukari.
Aidha, amefafanua kuwa kiwango
cha Mfumuko wa bei wa bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi
kwa mwezi Machi 2015 kimeongezeka hadi kufikia
asilimia 5.9 ikilinganishwa na asilimia 4.9 ya mwezi Februari 2015.
Akitoa ufafanuzi kuhusu
uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma kwa mwezi Machi
2015 amesema kuwa umepungua na kufikia shilingi 64 na senti 15 ikilinganishwa na
shilingi 64.59 za mwezi Februari 2015.
Kwa upande wa mfumuko wa
Bei wa mwezi Machi kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema una mwelekeo unaofanana
Uganda ikiwa na Mfumuko wa Bei wa asilimia 1.90 kutika asilimia 1.4 za mwezi Februari huku Mfumuko wa
Bei nchini Kenya kwa mwezi Machi 2015 ukiongezeka hadi kufikia asilimia 6.31
kutoka asilimia 5.61 za Februari.
0 comments:
Post a Comment